Watu wapatao 72 wameuawa na zaidi ya watu 800 wamekamatwa katika ghasia hizo zilizoanza kama maandamano alhamisi iliyopita kupinga kwenda jela kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma.
Aidha tume ya Umoja wa Afrika imelaani ghasia zinazoendelea Afrika Kusini zilizosababisha watu 72 kuuawa.
Waandamanaji waligeuza maandamano hayo na kuwa ghasia mwishoni mwa wiki, wakichoma moto, kufunga barabara kuu na kuvamia na kupora maduka.
"Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, amelaani vikali vurugu hizo ambazo zimesababisha vifo vya raia na matukio mabaya ya uporaji wa mali ya umma na ya kibinafsi, uharibifu wa miundombinu, ikiwemo kusitishwa kwa huduma muhimu katika eneo la Kwazulu-Natal, Gauteng na maeneo mengine ya Afrika Kusini," tume imeeleza katika taarifa yake.
Mamia ya wanajeshi yalitumwa kusitisha ghasia na uporaji Afrika Kusini kudhibiti machafuko hayo yaliyoibuka siku tano zilizopita.
"Mwenyekiti ametoa wito wa jitihada za haraka kufanyika ili kurejesha amani na utulivu katika taifa hilo kwa kuzingatia utawala wa sheria. Alifafanua kuwa kushindwa kufanya hivyo athari itakuwa kubwa si kwa taifa hilo pekee bali kwa ukanda wote ," tume iliandika katika taarifa yake.