GSM, Manji Waongeza Mzuka Yanga






WADHAMINI wa Yanga Kampuni ya GSM rasmi imekubali kufanya kazi pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji katika kuelekea msimu ujao.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Manji ahudhurie katika mkutano mkuu wa klabu hiyo wa kupitisha katiba mpya ya mfumo wa mabadiliko uliofanyika Jumapili iliyopita kwenye Ukumbi wa DYCCC, Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

 

Muunganiko huo wa GSM na Manji huenda ukaongeza hamasa ya wachezaji na mashabiki katika kuelekea dabi ya Simba dhidi ya Yanga.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Injinia Hersi Said, alisema kuwa mabadiliko ya Yanga siyo kwa ajili ya kumnufaisha mtu mmoja pekee, bali yapo kwa ajili ya kuinufaisha klabu.



Hersi alisema kuwa, wao GSM wapo tayari kushirikiana na kufanya kazi na Manji katika kuhakikisha wanafanikisha malengo yao ya kuijenga Yanga itakayokuwa tishio na mfano wa kuigwa barani Afrika.

 

Aliongeza kuwa wanatambua mchango wa Manji katika kuijenga Yanga itakayokuwa imara na kikubwa kuhakikisha wanachukua mataji yote ya ubingwa watakayoshiriki katika msimu ujao.

 

“GSM hatupo hapa kwa ajili ya kujinufaisha sisi tupo kwa ajili ya kuijenga klabu yetu ya Yanga na kikubwa tunataka kuifanya kuwa mfano wa kuigwa kama zilivyo baadhi ya klabu kubwa Afrika ambazo zimepiga hatua za kimafanikio.“

 

Hivyo tunamkaribisha Manji muda wowote kwa ajili ya kushirikiana kwa pamoja na hatimaye tufanikishe malengo yetu ya pamoja, ninaamini uwepo wake utaifanya klabu kufikia mafanikio mazuri.“

 

Siyo Manji pekee, milango ipo wazi kwa watu au makampuni mengine yatakayotaka kuja kuisaidia klabu yetu ya Yanga, tunatakiwa kufanikisha malengo tuliyojiwekea kwani timu inatakiwa kuwa na wawekezaji zaidi ya mmoja,” alisema Hersi.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad