Makamba Amkosoa Askofu Gwajima “Ni Hatari Kupotosha Watu”





Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
MBUNGE wa Bumbuli mkoani Tanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), January Makamba amesema, kauli aliyoitoa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu chanjo ya corona “ni hatari.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Makamba ambaye ni waziri wa zamani wa mawasiliano na teknolojia, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 26 Julai 2021, ikiwa ni siku moja tangu Askofu Gwajima ambaye naye ni Mbunge wa Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwaeleza waumini wa kanisa lao wasikubali kuchanjwa chanjo ya corona.

Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Makamba ameandika “kauli ya Askofu Gwajima kuhusu chanjo na dhamira ya Serikali kuleta chanjo nchini haikubaliki.”

“Ni hatari kupotosha watu wanaotuamini kuhusu mambo ambayo hatuna utaalam nayo. Mjadala kuhusu usalama wa chanjo ni sahihi lakini kiapo kwamba Serikali imeileta kuwadhuru watu si sahihi,” amesema Makamba.


Kauli ya Askofu Gwajima kuhusu chanjo na dhamira ya Serikali kuleta chanjo nchini haikubaliki. Ni hatari kupotosha watu wanaotuamini kuhusu mambo ambayo hatuna utaalam nayo. Mjadala kuhusu usalama wa chanjo ni sahihi lakini kiapo kwamba Serikali imeileta kuwadhuru watu si sahihi. pic.twitter.com/fUncsD9jQl

— January Makamba (@JMakamba) July 26, 2021

Akihubiri katika kanisa lake Ubungo mkoani Dar es Salaan jana Jumapili, Askofu Gwajima alishauri makundi matano yaliyopendekezwa na kamati ya corona iliyoteuliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, yasipewe chanjo hiyo, hadi tafiti dhidi ya athari hizo zitakapofanyika.

Makundi matano yaliyopendekezwa na kamati hiyo kuwa ya kwanza kupewa chanjo ya corona ni pamoja na, walinzi wa mipaka, viongozi wa dini, watumishi wa sekta ya afya na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

“…kwa nini mpaka sasa hakuna tafiti iliyofanywa na mtaalamu wa Kiafrika au Mtanzania, kuzungumzia madhara ya muda mrefu na mfupi ya anaye chanjwa. Msikubali kuchanjwaaaaa,” aliwaeleza waumini wake Askofu Gwajima

Tayari Tanzania imepokea msaada wa chanjo ya corona zaidi ya dozi milioni moja aina ya COVAX kutoka Marekani ikiwa ni uratibu wa Umoja wa Afrika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad