Hili Ndo Gari la Gharama Zaidi Duniani, Sawa na Nyumba 600




KUMILIKI gari zuri, yawezekana ni ndoto ya kila mtu duniani, pamoja na mambo mengine kama nyumba, ardhi, kazi na vitu vingine vya thamani.

Sasa aina gani ya gari, kwa ajili ya shughuli gani na la kiwango gani cha thamani inabaki kuwa jambo linalotenganisha kundi moja na lingine la wamiliki wa magari.

Wasanii, wanamichezo na watu wengine maarufu dunaini mara nyingi hutumia magari ya kifahari zaidi na yenye thamani kubwa kwa sababu ya shughuli zao na namna wanavyojiweka kwenye macho ya watu wanaowafuatilia.

Hata barani Afrika, inaonekana sasa kama kitu cha kawaida kwa watu maarufu wakiwemo wasanii, wafanyabiashara na wanamichezo kumiliki magari makali, ya kisasa na ya bei ya juu.


 

Mtandao wa Car mart Nigeria unamtaja David ‘Davido’ Adeleke kumiliki karibu magari 10 ya kifahari yakiwemo Rolls-Royce Cullinan 2019, Bentley Bentayga na Range Rover Sport.

Ayodeji ‘Wizkid’ Balogun pamoja na magari mengine anamiliki Lamborghini Uru na Porsche Panamera na msanii Diamond Platnumz wa Tanzania wiki hii ameonyesha gari yake mpya ya The 2021 Rolls-Royce Cullinan, kama moja ya magari yake ya kifahari likiwemo Cadillac Escalade.

Sasa yapo magari mengi tu ya kisasa, kifahari na ya thamani ya juu kama McLaren Speedtail, Pininfarina Battista, Mercedes-AMG Project One, Koenigsegg Jesko, Aston Martin Valkyrie, W Motors Lykan Hypersport, Pagani Huayra BC Roadster, Bugatti Chiron Pur Sport na Lamborghini Sian FKP 37.

Kwa mujibu wa mitandao mikubwa duniani kama Luxe.digital, motor 1 na wealthygorilla, magari yafuatayo yanatajwa kuwa ya gharama kubwa zaidi kwenye soko la sasa na kuyamiliki ni kasheshe.


6: Mercedes-Maybach Exelero – $8.0 milioni

Moja ya magari ya kifahari yenye gharama kubwa kuyamiliki kutoka Maybach. Gari moja la Maybach Exelero linagharimu dola milioni 8 na linaweza kwenda kwa mwenda wa kasi wa juu zaidi wa kilometa 351 kwa saa.

Kama umetazama video ya wimbo wa Lost One ya mwanamuziki maarufu duniani Jay-Z mwaka 2006 basi gari unaloliona la kisasa zaidi linaitwa Maybach Exelero. Gari hili limetoka toleo moja tu na linamilikiwa na Dr. Andre Action Diakite Jackson.


 
Dr. Andre ndiye aliyemkodisha Jay Z atumie wakati wa kutengeneza video ya wimbo huo. Matairi ya gari hii yana ukubwa wa inchi 21 yakitajwa kuwa ya kipekee katika aina ya magari yanayofanana na haya ya ‘sports cars’. Lina uwezo wa kubeba uzito wa mpaka kilo 2721.

Pamoja na uzuri wake, Mercedes ilitangaza kutozalisha tena aina hii ya magari na kujielekeza zaidi kwenye magari mengine ya kifahari ya S-Class.


5: Bugatti Centodieci – $9.0 milioni

Bugatti Centodieci inaendeleza kazi ya miaka 110 ya magari ya Bugatti yenye muundo mzuri na wa kuvutia. Moja ya magari yenye nguvu zaidi duniani ikiwa na horsepower 1,600. Ikileta historia yenye asili ya ufaransa, si nguvu tu bali hata thamani yake haishikiki, linauzwa kati ya $8.9 na $9.0 milioni.

Na mbaya zaidi toleo lake la sasa la mwaka 2021 ndilo toleo ghali zaidi kwani imepangwa kuuzwa magari 10 tu. Na tayari magari hayo 10 yameshapata wateja ambao wanayasubiria kwa hamu kukabidhiwa, wakiyanunua kila mmoja kwa thamani ya dola $9.0 milioni.

Inatajwa kuwa gari linalokwenda mwendo wa kasi zaidi likiwa kwenye barabara nyoofu na tambarare, lina mwendo wa kilometa 379 kwa saa ingawa ukifalinganisha na Chiron, yenyewe liko nyuma, ila kwa muundo wake na mvuto wake, kunafanya kuwa gari la kipekee.



4: Rolls-Royce Sweptail – $13milioni

Yapo matoleo mengi ya magari ya Rolls-Royce kuanzia Rolls-Royce – Ghost, Rolls-Royce -Wraith, Rolls-Royce -Cullican, Rolls-Royce Phamtom, Rolls-Royce 100EX mpaka Rolls-Royce Dawn lakini Rolls-Royce Sweptail ni toleo lenye thamani zaidi.

Kwa mara ya kwanza Rolls-Royce Sweptail kuzinduliwa ilikuwa Mei 2017 katika eneo la Concorso d’Eleganza Villa d’Este likiwa moja ya magari yanayotengenezwa ajili ya kukidhi mahitaji fulani ya wateja wake.

Ghari hili lililotengenezwa Uingereza lilitoka kama toleo la kipekee mwaka 2013 lakini sasa sokoni linatajwa kugharimu dola milioni $13. Kwa wanaofuatilia masuala ya magari, wanataja gari hili ndilo pekee lililoiweka Uingereza kwenye ramani ya nchi zenye magari ya kifahari, yenye muundo unaovutia na nguvu ya horsepower 453.


3: Pagani Zonda HP Barchetta – $17 Milioni


 
Magari mengine ya kifahari yanayotengenezwa na Kampuni ya Pagani ya Italia. Kampuni hii ilianza kuingiza sokoni magari ya Pagani mwaka 1999 na kusitisha uzalishaji mwaka 2019, na mpaka inasitisha ilikuwa tayari imezalisha magari 140. Iliamua kusitisha na kujielekeza zaidi kwenye aina nyingine ya magari ya ‘Huayra.

Zonda HP Barchetta lilikuwa toleo lake la mwisho lililokuwa na kipekee kabisa. Italia gari hili linaitwa ‘boti ndogo’ kwa namna muundo wake ulivyo na uwezo wake wa kupita sehemu mbalimbali licha ya kuonekana ni gari ‘mayai’.

Ni gari fupi mno lenye urefu wa nusu mita tu lakini lina kasi ya kilometa 355 kwa lisaa. Bahati mbaya pia ni kwamba Zonda HP Barchetta ambayo yalikuwa na upekee kuliko magari mengine chini ya Pagani yalitengenezwa matatu tu na gari ya mwisho iliuzwa kwa dola milioni $17.6 na kufanya kuwa moja ya magari yenye thamani zaidi duniani.


2: Bugatti La Voiture Noire – $18.7 Milioni

Magari ya Bugati yamekuwepo kwa zaidi ya miaka 100 sasa. Inachokifanya kampuni hiyo ni kuongeza nakshi na kubuni aina mpya kwa mahitaji ya sasa.

Mfano Bugatti La Voiture Noire, ni tafsiri ya gari binafsi la Jean Bugatti aina ya 57 SC Atlantic ambalo lilitoweka baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Lilitengenezwa mwaka 1934 na Jean Bugatti, mtoto mkubwa wa mwanzilishi wa kampuni hiyo, Ettore Bugatti, sasa limerejea lakini kwa namna ya kipekee kwa kuongezwa ubunifu wa kuvutia na kuwa moja ya magari ya bei ya juu kabisa kuwahi kuuzwa. Limeuzwa kwa dola $19 million.


Kwa kukadiria tu thamani ya gari moja la Bugatti La Voiture Noire unaweza kujenga karibu nyumba 400 za kiwango cha kati zenye vyumba vinne na kila kitu ndani. Ukithaminisha nyumba hiyo kwa thamani ya dola 45,000 mpaka 55,000 kwa moja.

Lina horsepower 1500 na mwendo kasi wa kilometa 420 kwa saa. Tangu kununuliwa kwa bei hiyo mwaka 2019 mpaka sasa hakuna toleo lingine la gari ya kifahari lililotolewa na kuipiku La Voiture Noire kwa gharama na kuongoza kwa mara ya pili mfululizo kama gari lenye thamani zaidi duniani. Kuzinduliwa kwa Rolls-Royce Boat Tail Mwezi May mwaka huu kutaiondosha Bugatti La Voiture Noire kwenye chati ya kuwa juu gari lenye thamani ya juu duniani.


1: Rolls-Royce Boat Tail – $28.0 Milioni

Wengi wanaweza kuishia kwenye Bugatti La Voiture Noire kama gari lenye thamani zaidi, lakini lipo gari jipya linaloingia sokoni sasa kutoka Rolls-Royce linaitwa Rolls-Royce Boat Tail. Ni toleo la kipekee ambalo kwa miaka minne limekuwa likitengenezwa muondo na muonekano wake. Ukilitaka gari hili lenye friji mbili ndani litatengenezwa kwa mahitaji yako yakiwemo ya rangi.



Injini na chesesi yake ni kama toleo la Rolls-Royce Phantom. Ingawa haijathibitishwa, inaelezwa kuwa Jay Z na mkewe Beyonce ndio walioweka oda ya kutengenezewa gari hili. Lakini taarifa rasmi ni kwamba yatatengenezwa magari matatu tu ya Rolls-Royce Boat Tail 2021 na moja litauzwa kwa dola $28.0 Million.

Thamani ya magari yote hayo matatu inaweza kuwa sawa na nyumba za kawaida karibu 600 au simu ndogo za kitochi (mulika mwizi) zaidi ya 1,120,000 kwa thamani ya dola 25 kwa simu 1.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad