Moshi. Mji wa Moshi unazizima, ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mfululizo wa vifo vya watu wenye umaarufu waliofariki ndani ya wiki moja, katika hospitali za mkoa wa Kilimanjaro.
Watu wanane mashuhuri katika mji wa Moshi wamefariki dunia kutokana na maradhi ambayo hayakuwekwa wazi, huku vifo vyao vikiwa gumzo katika mitandao ya kijamii kutokana na vifo hivyo kufuatana.
Familia ya wafanyabiashara inayofahamika ‘The Big Family’ imepoteza wanachama wake watatu ndani ya siku saba, ambao ni mfanyabiashara Stanley Shayo anayemiliki kampuni ya Tanganyika Tours na baa ya Kwetu Longe.
Mwenyekiti wa bodi ya The Big Family, Christopher Shayo jana alithibitisha kuondokewa na wanafamilia watatu ndani ya wiki moja na kwamba jana asubuhi alifariki Soren Kaale, aliyewahi kuwa meneja mkuu wa Moshi Timber Utilization.
“Ni kweli zimekuwa siku mbaya kwetu. Leo hii (jana) tumempoteza Soren Kaale na ndio nimetoka KCMC muda huu. Juzi hapa tumempoteza Stanley Shayo tena tumempoteza katikati ya majonzi ya kumpoteza Boniface Ngowi,” alisema.
Mbali na hao, lakini juzi asubuhi zilisambaa taarifa ya kufariki kwa diwani wa kata ya Kileo Wilaya ya Mwanga, Salim Zuberi aliyefariki katika hospitali ya St Joseph na kifo chake kulithibitishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga, Zefrin Lubuva.
“Tumempoteza kiongozi wetu. Niwaombe wananchi wa kata ya Kileo wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu, lakini niendelee kuwasisitizia wachukue tahadhari dhidi ya virusi vya corona kwa vile eneo letu ni la mpakani,” alisema.
Wiki hii pia wakazi wa mji huo walitikiswa na kifo cha mmiliki wa duka kubwa la dawa za binadamu la Pharm Source lililopo jirani na Nyumbani Hoteli, Doreen Njau au Ashura Mshana na kifo chake kilitikisa mitandao ya kijamii nchini.
Mbali na mfanyabiashara huyo, lakini kifo cha Ofisa Afya katika kituo cha Forodha cha Holili, Edward Ocheing nacho kiliibua mshtuko, hasa ikizingatiwa kifo chake kilitokana na kujisikia tu vibaya na hakuchukua muda mrefu alifariki dunia.
Jana mji wa Moshi uligubikwa na taarifa za simanzi za kifo cha aliyewahi kuwa mkuu wa Idara ya Mazingira ya Manispaa ya Moshi, Danford Kamenya aliyehamishiwa Jijini Mwanza kikazi ambako ndipo umauti ulipomkuta jana.
Mbali na msiba huo, jana hiyo hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alimpoteza ndugu yake aitwaye Charles Mbowe, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alilithibitishia gazeti hili juu ya kufariki kwa Charles na kwamba alikuwa amelazwa KCMC kwa muda wa wiki moja sasa akipatiwa matibabu kabla ya umauti kumkuta jana asubuhi.