Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile amesema wizara hiyo imejipanga kuhakikisha kwa miaka mitano inajenga uchumi wa kidigitali. Dk Ngugulile ameyasema hayo leo Alhamisi Julai Mosi 2021 jijini Dodoma katika uzinduzi wa tovuti ya wizara hiyo pamoja na mpango mkakati wa 2021/26.
Amesema kwa miaka mitano wanaenda kuboresha mkongo wa Taifa kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano ili yaweze kufika katika wilaya zote nchini pamoja na nchi jirani.
“Tumejipanga kuweka mazingira wezeshi ya biashara mtandao na kazi hii ilishaanza, vijana wanatambua mtu anaagiza mzigo wake anapiga picha na kusambaza kwa ajili ya kupata wateja na wakati mwingine anampelekea hadi alipo,” amesema Dk Ndungulile.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Shirika la Posta ina mpango wa kuikuza vizuri na kuirasimisha ili watu waweze kufanya biashara vizuri na sasa hivi imejipanga kuboresha anuani za makazi.
“Tunataka kila nyumba kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Idara za mipango miji, Tamisemi na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha tunaweka mipango miji mizuri kwa kuboresha barabara mitaa na namba za nyumba.”
OPEN IN BROWSER