WAKATIwakisubiriwa kukabidhiwa kombe lao la ubingwa, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes Da Rosa haifikiri kabisa mechi yake ya mwisho katika ligi dhidi ya Namungo kutokana na mipango yake kuwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la azam Sports (ASFC), maarufu kama FA dhidi ya Yanga huku akiwataka nyota wake wakiwemo Luis Miquissone na Clatous Chama wapambane kuipa ushindi timu hiyo.
Simba ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni mara ya nne mfululizo lakini pia ni mabingwa watetezi wa Kombe la FA, wanatarajia kucheza na Yanga Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Gomes alisema kuwa baada ya kufanikiwa kutetea ubingwa wa ligi kuu, kwa sasa mipango yake inaelekea Kigoma katika mchezo wa fainali dhidi ya Yanga huku akiwataka baadhi ya nyota wake kutambua thamani ya mchezo huo kwa kuhakikisha wanapata ushindi.
“Nadhani kuhusu ligi, nimeshafunga hesabu kwa sababu tayari ni mabingwa na bado tuna mechi za kucheza mkononi, tunasubiria kupewa ubingwa wetu, japokuwa bado kuna kazi ya kufanya kuelekea kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Yanga ambao kwetu una umuhimu wa kupata ushindi.“
Unajua sisi ni mabingwa watetezi, tunaenda kucheza na Yanga katika mchezo ambao naamini utakuwa mgumu kutokana na timu tunayocheza nayo lakini tayari nimekuwa nikiongea na wachezaji wangu kama Chama, Miquissone, Bocco juu ya kitu gani ambacho nahitaji kuona kinatokea kwenye huo mchezo ila jambo kubwa ni kutetea ubingwa licha ya kucheza na timu ngumu,” alisema Gomes
Ibrahim Mussa,Dar es Salaam