MAJEMBE mapya ya Yanga, mshambuliaji Fiston Mayele na beki wa kulia, Shabani Djuma, wamefunguka kuwa wataushuhudia mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Yanga na Simba kupitia runinga.
Leo Jumapili, Yanga na Simba zinatarajiwa kumenyana kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo mkoani Kigoma.
Mayele na Djuma hapo awali ilisemekana wataingia nchini mapema kwa ajili ya kuuwahi mchezo huo na kuushuhudia moja kwa moja wakiwa uwanjani, kabla ya uongozi wa Yanga kubadilisha maamuzi juu ya kutua kwao hapa nchini.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meyele alisema yeye na Djuma watautazama mchezo huo kupitia runinga wakiwa kwao nchini DR Congo, huku mshambuliaji huyo akiiitakia ushindi Yanga katika fainali hiyo.“
Tutautazama mchezo wa Yanga na Simba kupitia TV, mara zote tumekuwa tukiifuatilia Yanga, naamini Yanga itaenda kuibuka na ushinda na natamani hili liweze kutimia.“Kuhusu kuja Tanzania tulikuwa tunasubiri mchezo huu wa fainali umalizike kwanza kisha ndiyo tuje, hivyo baada ya kumalizika tutakuja Tanzania,” alisema mshambuliaji huyo.