Dar es Salaam. Licha ya Serikali kusisitiza utekelezaji wa tozo mpya ya miamala ya kwenye simu inayoanza kutozwa kuanzia kesho, wananchi wameonyesha wasiwasi kutokana na gharama mpya za kutuma au kutoa fedha.
Kuanzia kesho Alhamisi Julai 14, 2021, wanaotuma au kutoa fedha kwa wakala wa simu ya mkononi wataanza kulipia kodi ya uzalendo ambayo ni kati ya Sh10 na Sh10,000 kulingana na ukubwa wa muamala.
Kutokana na kodi hiyo mpya, wadau wana wasiwasi kwamba itapunguza matumizi ya huduma hiyo hivyo kushusha mchango wake kwenye uchumi.
Kwa gharama mpya zilizopo, wapo wanaoamini hakuna atakayeenda kwa wakala kufanya muamala.
Kabla ya kodi ya uzalendo, wateja wa Airtel Money walikuwa wanakatwa Sh350 tu ndani ya mtandao kutuma Sh15,000 lakini sasa watalipa Sh960 na walikuwa wanakatwa Sh550 kwenda mtandao mwingine lakini imepanda mpaka Sh1,160. Watakapotaka kutoa, watalipia Sh2,010 badala ya Sh1,400 ya mwanzo.
Kwa wateja wa Mpesa, kutuma Sh15,000 kwenda kwa mteja asiyesajiliwa, makato yatakuwa Sh970 kutoka Sh360 wakati ikigharimu Sh2,820 kwa mteja asiyesajiliwa kutoka Sh2,210. Kwenda mitandao mingine, kiasi hicho kitalipiwa Sh1,160 kutoka Sh550 iliyokuwapo na watakaopelekwa kwenye akaunti zao za benki watakatwa Sh1,810 badala ya Sh1,200 iliyokuwapo. Kutoa kiasi hicho iwe kwa wakala au ATM, watakatwa Sh2,060 kutoka Sh1,450.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT), Sosthenes Kewe anasema kwa kuwa miundombinu ya huduma hizi imeshawekwa na matumizi ya simu yamekuwa sehemu ya maisha ya wananchi, mabadiliko ya tabia za wateja ndio yatakayoamua uendelevu wa kodi hii mpya.
“Wapo wanaokopa au kuweka akiba kwenye simu zao. Wapo wanaolipia usafiri mfano Uber kwa simu zao. Adhima ya kuwa na uchumi wa kidijitali unataka watu wengi zaidi kutumia huduma za fedha. Ongezeko la gharama linaweza kuwarudisha watu kulipa kwa fedha taslimu,” anasema.
Kwa mabadiliko haya mapya, mteja wa miamala kwa simu ya mkononi atakuwa analipa kodi tatu. Kwanza ni ushuru wa forodha ambao ni asilimia mbili na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Hizi mbili zilikuwepo kabla ya mabadiliko yanayoanza leo.
Kwenye makato ya Sh360 yalikuwapo kutuma Sh15,000 kwa mteja asiyesajiliwa, Vodacom ilikuwa inapata Sh289.1 na Serikali kukusanya Sh65 VAT na Sh5.9 ya ushuru wa forodha lakini kuanzia kesho Serikali itakuwa inaondoka na Sh680.9 ilhali Vodacom ikibakiwa na ileile.
Akizungumza kwenye kipindi cha 360 cha kituo cha runinga chaa Clouds, Julai 12, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema “hii sio tu ni kodi bali tunatunisha mfuko wa mshikamano. Tutachangia kupitia makato ya simu.”
Waziri huyo alisema itakuwa aibu kwa miradi ya maendeleo kukwama kwa kuwa tu Serikali imeshindwa kukusanya kodi hivyo akavitaka vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kodi kwa maendeleo yao.
“Kuna mambo hayapaswi kuwepo. Haitakiwi kuona kijiji hakina barabara inayopitika muda wote na tunabeba wagonjwa juujuu. Mbona tunaweza miito ya simu na kukatwa hela nyingi tu kwa nini isiwe kutunisha mfuko wa mshikamano?” alihoji Waziri Mwigulu.
Kutokana na vipeperushi vya makato mapya yatakayoanza usiku wa kumkia kesho, Boniface Mekuru amesema “Naenda kutoa salio lote nililonalo kabla ya kesho. Haya makato hayavumiliki. Nikikatwa Sh8,000 tu huwa naumia sasa haya mapya, siwezi kuyavumilia.”