MENEJA wa Timu ya Mbeya City, Mwegane Yeya, amesema kikosi hicho kinapambana kuhakikisha kinaibuka na ushindi kwenye mechi mbili zilizobaki kwenye Ligi Kuu Bara ambazo ni sawa na dakika 180.
Mbeya City inapambana kujinasua na janga la kushuka daraja ambapo inahitaji pointi sita ili kufufua matumaini ya kubaki kwenye ligi. Tayari kikosi hicho kimekusanya pointi 36 kwenye mechi 32.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mwegane alifunguka kwamba: “Tumebakiwa na mechi mbili kumaliza ligi dhidi ya Gwambina na Biashara United, ni mechi ambazo tutamaliza nyumbani, hivyo ni lazima tupambane kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ili tujihakikishie nafasi ya kubaki kwenye ligi.
“Hatupo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo, hivyo tutapambana kwa jasho na damu kwenye mechi hizi ili tuwe sehemu salama.”
Mbeya City inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 36 baada ya kushuka dimbani mara 32, imeshinda mechi nane, sare 12 na kupoteza 12.