Mbunge Ditopile amuunga mkono Rais Samia kwenye tozo ya miamala ya simu





MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amewataka watanzania nchini kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa wazalendo katika kulipa kodi kwani uimara na ukuaji wa Taifa lolote kiuchumi hutokana na ulipaji wa kodi.

Ditopile ametoa kauli hiyo leo alipokua akitoa maoni yake kuhusu bajeti ya fedha ya mwaka huu hasa katika eneo la tozo za miamala ya simu ambapo ameunga mkono ukusanyaji huo akisema utasaidia kukuza uchumi wa Nchi.

Amesema pia kumekuepo na upotoshaji wa baadhi ya watu wasio na nia njema wakidai kuwa tozo za laini ya simu ni kila mtu anapoongeza Salio jambo ambalo ni kinyume na ilivyotangazwa na serikali.

" Kumekua na upotoshaji mkubwa unaofanywa na watu kwamba tozo za laini ni kila unapoweka salio huu ni uongo kwani tozo hii ya sh 10 hadi 200 zitatozwa mara moja tu kwa mwezi pale Mtu anapoongeza salio, siyo kila unapoweka bali ni mara moja tu kwa mwezi.

Watanzania wanapaswa kumuunga mkono Rais wetu Samia katika hili la ukusanyaji wa kodi za miamala kwani litasaidia kuirudisha Nchi yetu katika uchumi imara, tukumbuke wakati Rais anahutubia Bunge alitueleza wazi kuwa uchumi wetu umeshuka kutoka asilimia 6.9 hadi 4.7 kutokana na athari ya janga la Corona hivyo ni lazima Serikali ichukue hatua za kurejesha uchumi wetu," Amesema Ditopile.

Amesema fedha zinazotokana na makato hayo ya miamala na tozo za salio ndio zinazoenda kuchochea miradi ya maendeleo ikiwemo kujenga miundombinu ya barabara, uboreshaji wa elimu na sekta ya afya.

" Bila kumuunga mkono Rais Samia katika ukusanyaji wa kodi hatuwezi kumsaidia kuendesha Nchi, hizi fedha zinazotokana na makato haya siyo faida tu kwa Serikali bali ni kwetu sisi wananchi, sisi Bungeni ni mashuhuda wa kila Mbunge wa Jimbo amepatiwa Sh Milioni 500 kwa ajili ya barabara, bila kulipa kodi hizi fedha hatuwezi kuzipata," Amesema Ditopile.

Amewaomba watanzania kutosikiliza maneno ya wanasiasa badala yake waiunge mkono Serikali yao kwa kulipa kodi ambayo ina mchango katika kuboresha Vituo vya Afya na Zahanati ili kuendelea kuokoa maisha ya Mama Mjamzito na Mtoto wakati wa kujifungua.

" Ulipaji huu wa kodi ndio utamsaidia Mama Samia kutekeleza azma yake ya msingi ya kumaliza changamoto ya maji na kumtua Mama Ndoo, tulimsikia akisema kuwa yeye ni Mama Maji anataka kuona kero ya maji inaisha nchini, ili afanikiwe katika hilo ni sisi kumuunga mkono katika kulipa kodi," Ameongeza Ditopile.

 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad