Mwanasiasa mashuhuri nchini ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje akiwa CCM na mwaka 2020 kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo, Bernard Kamilius Membe amepata ajali ya gari leo Julai 8, 2021 akitokea nyumbani kwake Rondo kuelekea Lindi.
Kwa mujibu wa msaidizi wake amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 7:30 mchana lakini Membe alitoka salama wala hakuna aliyeumia kutokana na ajali hiyo.
Global Digital imezungimza kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, na hiki ndicho alichokisema;
“Ni kweli ajali hiyo imeripotiwa majira ya mchana, dereva akathibitsha kuwa gari hilo ni mali ya mheshimiwa na mheshimiwa alikuwemo kwenye gari.
“Sisi kama Jeshi la Polisi hatujamkuta Membe eneo la tukio, tumemtafuta lakini juhudi hazijazaa matunda. Kwa hiyo hatuwezi kuthibitisha kwamba amepata ajali sababu hatuna uthibitisho kama alikuwemo kwenye gari wakati ajali ikitokea.
“Tunaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali kama ni uzembe wa dereva ama ni ajali iliyosababishwa na gari kupata hitilafu,” amesema RPC wa Lindi.