MIILI ya watu watano akiwemo mwanafunzi wa kidato cha nne waliokuwa wakihofiwa kufa maji Wilayani Singida imepatikana na kuopolewa baada ya juhudi za askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutoka mikoa mitano kushirikiana na wavuvi eneo hilo.
Watu hao watano waliokuwa wakisafiri na mtumbwi wa kienyeji kuelekea kwenye msiba kijiji cha Kinyento na kuzama Juni 5, mwaka huu majira ya asubuhi, walifariki baada ya mtumbwi ulikouwa ukiwavusha kuzama katika Bwawa la Ntambuka Kata Kinyeto.
Watu hao watano ambao wamepatikana wakiwa wamekwishafariki ni Ayubu Mohamed (39) Abubakar Hassani (25) Abubakar Hamisi (35) Hamisi Ali (30) na Ali Hamisi (18) ambaye ni mwanafunzi katika shule ya Sekondari Mrama Halmashauri ya wilaya Singida.
Taarifa za Jeshi la Zimamoto jana zilieleza kuwa katika mtumbwi huo walikuwemo watu saba ambapo wawili kati yao akiwepo nahodha waliokolewa na kukimbizwa hospitali kwa matibabu huku wakibakia watu watano ambao miili yao imepatikana jana kwa jitihada za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Katika taarifa za awali zilizotolewa na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (SACF) Ivo Ombella alisema chanzo cha ajali hiyo ni mtumbwi huo kupigwa na mawimbi makubwa katika bwawa hilo.