SERIKALI imepokea msaada wa chanjo ya Corona kutoka Marekani na kueleza kuwa baada ya kujiridhisha kuwa ni salama utolewaji wake utafanyika nchi nzima lakini kwa kuanza na mikoa 10 ya kipaumbele.
Mikoa hiyo ya kipaumbele ni Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Kigoma, Singida, Dodoma, Iringa na Mtwara.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kupokea msaada wa dozi zaidi ya milioni moja za chanjo ya corona aina ya Johnson & Johnson.
Alisema msaada huo umetolewa na Marekani ikiwa sehemu ya ahadi ya nchi hiyo ya kutoa angalau dozi milioni 25 kwa Afrika kati ya dozi milioni 80 zilizoahidiwa kwa bara hilo.
Waziri huyo aliishukuru Marekani kwa mchango mkubwa wa kutoa chanjo kwenye mpango wa COVAX Facility ambao umewezesha Tanzania kuwa nchi mojawapo kupata dozi 1,058,400 zitakazosaidia kupambana na corona.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha angalau asilimia 60 ya Watanzania wanapata chanjo hata baada ya hizo kutumika.
“Chanjo hii itaanza baada ya watalaamu kujiridhisha, wataalamu wetu wanafanya taratibu za kujiridhisha kabla ya kuanza mchakato wa kuchanja. Ninawaomba wananchi wajitokeze pindi tukianza,” alisema.
Dk. Gwajima alisema serikali itapokea chanjo ya aina nyingine katika wiki zijazo ili kuhakikisha watu wote wanapata huduma hiyo na kipaumbele kikiwa ni wahudumu wa afya, watu wazima kuanzia miaka 50 na wenye magonjwa sugu katika mikoa hiyo 10.
“Tunaendelea kuchukua tahadhari zote dhidi ya corona kwa kuzingatia afua zote na sasa tujiandae kupata afua ya chanjo kama silaha bora.
"Afua ya chanjo siyo jambo jipya, Tanzania imekuwa ikipokea chanjo miaka mingi kwa ajili ya kudhibiti magonjwa,” alisema.
Waziri huyo alisema ujio wa chanjo hiyo umefuata taratibu zote ambazo serikali imekuwa ikitumia kujiridhisha kuhusu mapokezi ya bidhaa za afya.
“Kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais John Magufuli, ilielekeza kuwa ‘Wizara ya Afya ijiridhishe kabla ya kupokea chanjo hizo’, wizara haitapokea chanjo hadi ijiridhishe,” alisema.
Dk. Dorothy alisema kuwa kupitia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, wizara imetimiza wajibu wa kujiridhisha.
Alisema mara baada ya kujiridhisha, serikali itaanza kutoa chanjo hiyo katika vituo mbalimbali vya afya kwa mujibu wa miongozo iliyopo na kuwataka wahusika kuwajibika ili Watanzania waipate.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Abeli Makubi, alilishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na WHO kwa kufanikisha Tanzania kupata shehena ya dozi hiyo ya kwanza.
Balozi wa Marekani nchini, Dk. Donald Wright, alisema msaada wa chanjo utasaidia kuwalinda Watanzania dhidi ya corona na kupunguza vikwazo katika jitihada za kuujenga upya uchumi wa Tanzania.
Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Shalini Baliaguna, aliitaka jamii kujiepusha na uvumi unaotangazwa mitandao ya kijamii kuhusu corona na kutaka watu watafute taarifa sahihi vyanzo rasmi.
Mwakilishi Mkazi wa WHO, Dk. Tigast Mengistu, alisema Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa mbele kwa kuwachanja watu wake.
Alisema wapo tayari kusaidia Tanzania kuhakikisha chanjo inawafikia watu wote waliopo.