Mitungi ya Tesi yaibua Taharuki




MLIPUKO wa mitungi ya gesi umezua taharuki kwa wakazi wa Tabata wilayani Ilala jijini Dar es Salaam baada moto mkubwa kuzuka na kusababisha athari kubwa ikiwamo kuunguza shule ya awali.

Kishindo cha mlipuko huo kilisikika usiku wa kuamkia jana, huku mashuhudua wakidai wananchi waliingiwa na taharuki na kukimbia ovyo na wengine kulazimika kuruka ukuta na kupata majeraha.

Vilevile, walidai mmiliki wa duka la mitungi hiyo ya gesi waliyemtaja kwa jina moja la Shayo, akizirai baada ya kupata taarifa hiyo.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa tano, moto mkubwa ukiibuka na kuleta madhara ikiwamo kuiunguza sehemu ya Shule ya Awali ya Destiny iliyoko jirani na duka hilo.

Madhara mengine ni mtungi kutoboa ukuta wa nyumba jirani na mwingine kuvunja kioo cha gari.


Mama Shayo, anayeishi jirani na duka hilo, alisema mmiliki wa duka hilo baada ya kupata taarifa hizo alianguka na kupoteza fahamu, hivyo kuwahishwa hospitalini.

“Mwenye duka baada ya kupewa taarifa alipoteza fahamu na amekimbizwa hospitali. Hili ni duka kubwa, alikuwa anauza vitu mbalimbali ikiwamo hizi gesi na pembeni kuna genge.

"Lilikuwa linahudumia mtaa mzima, pengine amechukua mkopo au ndiyo kitega uchumi chake," alidai.


Alisema madhara ni pamoja uharibifu wa duka husika, shule na baadhi ya mitungi kuruka na kuvunja ukuta na kupasua kioo cha gari.

"Tulikuwa tumelala tukasikia mitungi kama inapiga kelele, baada ya hapo tukasikia inalipuka halafu inaruka, tulipotoka tukakuta moto umeenea ndipo tukatafuta watu wa TANESCO (Shirika la Umeme) na Zimamoto (Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)," alisema.

Mama Shayo alidai Zimamoto walichelewa kufika eneo la tukio na walipowasili, ilishindikana kuuzima moto kwa haraka kutokana na kuishiwa maji.

Alisema kuwa wakati mitungi hiyo inalipuka, baadhi ya watu walidhani ni majambazi na wakawa wanakimbia ovyo.


Shuhuda mwingine, Issa Mbowe, alisema alilazimika kuruka ukuta baada ya moto kuwa mkubwa na kuumia sehemu ya mkononi na mguuni.

"Nilishindwa kutokea getini kwa sababu moto ulikuwa mkubwa, wakati ukitokea nilikuwa nimeshalala lakini kelele za mlipuko ndiyo ziliniamsha.

"Sisi ni wapangaji wawili tuliruka ukuta na wengine walibaki ndani wakitafuta namna ya kujitetea," alisema.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Mkoa wa Ilala, Erisa Mugisha, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo alipotafutwa na Nipashe jana mchana.


Alisema madhara makubwa yametokea kwenye duka hilo na vyumba vingine sita vya shule hiyo ya awali vimeungua kwa kiwango kikubwa.

“Moto ulianzia katika duka hilo ambalo lina genge pia, na baadaye kusambaa shuleni na kusababisha mitungi 18 kuruka sehemu mbalimbali. Chanzo chake bado hakijafahamika kama walikuwa wanapika au la," alisema.

Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo, alisema kwa ujumla wauzaji wa gesi wanatakiwa kuhakikisha eneo linalohifadhi mitungi hiyo linakuwa lenye kuiwezesha kupumua.

“Huwa tunawaambia kwamba mitungi inatakiwa kuwekwa eneo la peke yake, yaani linakuwa maalum kwa ajili ya mitungi ya gesi.

"Liwe eneo linaloleta hewa ili mitungi iwe inapumua. Kama anaweka ndani, hilo ni tatizo. Wanafanya biashara bila kufuata masharti na mwisho wa siku wanaumia wao," alionya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad