MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Abdoul Razack, amefungasha kila kitu kilicho chake, kisha kutimka kambini, huku akijiandaa kutimkia kwao Burundi.
Mrundi huyo ambaye alisaini kandarasi ya miezi sita kuichezea Yanga, mkataba wake huo umemalizika rasmi jana Jumatatu, hivyo akachukua uamuzi huo haraka sana
Tangu ajiunge na Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu huu, Fiston amefunga mabao mawili katika michuano yote ambapo moja Ligi Kuu Bara na lingine Kombe la FA.
Akizungumza na Spoti Xtra, Fiston amesema kuwa: “Nilimwambia injinia (Hersi Said) kuwa Julai 12 mkataba wangu unaisha, hivyo naondoka, nilimwambia hivyo usiku ule tulipokuwa tunapata chakula cha usiku (Jumamosi iliyopita).
“Alinisisitiza kubaki mpaka mwisho wa msimu kwa sababu ligi imechelewa kuisha, ila nikakataa, naona bora nirudi nyumbani maana mkataba wangu umeisha.“
Hivyo leo (jana) nimechukua kila kilicho changu, nimeondoka kambini na kurudi nyumbani. Hivi karibuni natarajia kwenda kusalimia wazazi nyumbani Burundi.”