Baada ya mwanariadha Sha’Carri Richardson kuenguliwa kwenye mbio za Mita 100 kwenye michuano ya Olimpiki 2020 ambayo itaanza Julai 23, mwaka huko Tokyo, Japan na sababu kuu ya kuenguliwa kwake ikiwa ni baada ya kufanyiwa vipimo na kubainika kuwa anatumia bangi, rapa P Diddy wa Marekani ameshusha tuhuma nzito dhidi ya wazungu.
P Diddy amesema anakerwa na watu mbalimbali hasa wazungu ambao wamekuwa wakimnanga Sha’Carri mitandaoni akiwemo mwandishi mmoja kutoka Australia ambaye alikwenda mbali zaidi na kudai mwanadada huyo ni feki kama zilivyo nywele na kucha zake.
P Diddy kupitia ukurasa wake wa Instagram anawalaumu wote wanaomnanga mwanadada huyo na kusema kuwa bangi haimfanyi mtu awe na mbio zaidi kama baadhi ya watu wanavyodhani kuwa mwanadada huyo amekuwa akishinda kutokana na kutumia bangi.
P Diddy ameshusha shutuma nzito kwa wazungu akisema kuwa amechoka kuwaona wazungu wanakaa na kutunga sheria ngumu ambazo ni kwa ajili ya kuharibu na kudidimiza ndoto na malengo ya mtu mweusi, wakiwachukulia kama watumwa.
Pia P Diddy ameendeleza kampeni yake ya kumtetea mwanadada huyo kupitia hashtag ya #LETHERRUN akisema kuwa mamlaka kubwa zimekuwa zikitumia mbinu hii kutokomeza ndoto za mtu mweusi hususan wanamuziki, waigizaji na wengi waliopo katika kiwanda cha burudani.
Kwa ufupi P Diddy haamini kama bangi inamfanya mtu kufanya vitu vya ziada na huo ndiyo ukweli kwa mujibu wake, anaamini kuwa bangi inatumiwa kama fimbo ya kumwadhibia mtu mweusi.s
STORI NA SIFAEL PAUL | GPL