Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kulinda amani na utulivu wa nchi kwani kuna chokochoko zimeanza akiwataka wananchi kuzipuuza na kutozipokea.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 7, 2021 aliposimama katika Stendi ya mabasi ya Msamvu mkoani Morogoro kuwasalimia wananchi wa mkoa huo. Samia ameanza ziara ya siku mbili mkoani humo.
Bila kueleza kwa kina kuhusu chokochoko hizo, Samia amewataka wananchi kuhakikisha wanailinda amani na utulivu wa nchi ili viongozi waendelee kufanya kazi.
Ameonya kuwa kumekuwa na baadhi ya watu wanaofanya chokochoko hali inayoashiria uvunjifu wa amani, “tuendelee kulinda amani na utulivu wa nchi yetu, amani iliyopo itawezesha viongozi kufanya kazi vizuri.”
“Vijichokochoko vimeanza naomba msivipokee, wanaokuja na hivyo walishajua matumbo yao yanajaaje, chakula chao wanatoa wapi, fedha za matibabu wanatoa wapi nawaomba sana wasiwaingize kwenye huo mkenge kwa sababu pakichafuka ni wewe na familia yako mtakaa ndani msijue chakula mtatoa wapi na wala usijue mtoto akiumwa utamtibu kwa fedha gani,” amesema.
“Niwaombe sana ndugu zangu tulinde amani yetu nchi yetu itulie na tulinde ajira zipatikane na mambo mengine yaendelee.”