Rais Samia "Watanieleza Hizo Bilioni 1 Wamepeleka Wapi"




RAIS Samia Suluhu, amesimama barabarani eneo la Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro kusikiliza kero za wananchi wa eneo hilo ambalo ni jimbo la Profesa Palamagamba Kabudi.

“Mambo yanayomgusa mwananchi moja kwa moja; maji, elimu, afya, umeme, barabara za vijijini ili kusafirisha mazao tunakwenda kuyasimamia, tutayatekeleza kama yalivyo kwenye Ilani ya Uchaguzi, maendeleo ni hatua, tumeanza na tunakwenda polepole, tutafika.

“Hapa Kilosa nimeambiwa kuna shida ya umeme kuwa mdogo na kukatika katika, tutakwenda kukaa na Mbunge na Waziri wa Nishati tuone namna ya kulitatua. Kuna mradi hapa wa kuongeza voltage za umeme, ninaamini mradi ule ukikamilika umeme utaongezeka.

“Nimeambiwa Barabara ya Km 71 inayotoka Miyobo, kwenda Lumuma hadi Kidete ni muhimu sana, tunakwenda kuitekeleza kama ilivyo kwenye Ilani ya Uchaguzi. Kama tunajenga Barabara kubwa, Km 71 sio kitu, tunakuja kuijenga.


“Barabara za vijijini ambazo zipo chini ya TARURA, tumeongeza Tsh 100 kwene kila Lita ya mafuta ili tukusanye zikatusaidie kujenga barabara zenye ubora vijijini.

“Mimi najiita ni mama maji, nasikitika kuona akina mama wanateseka kutafuta maji, akina baba mnawatoa wanawake alfajiri kwenda kutafuta maji, wakichelewa mnawakong’ota, jambo ambalo si haki, nakwenda kutafuta pesa kuja kutekeleza miradi ya maji.

“Tumetumia zaidi ya sh bil 1 kujenga miundombinu ya maji na kuchimba visima, visima vile havina maji. Mainjinia nakula nao sahani moja, wanieleze kwa nini wametumia bil 1 kuchimba visima na havitoi maji, ni sawa na kutumbukiza pesa chooni. Watafika kwangu wanieleze.

“Nimeambiwa kuna mafuriko huwa yanatokea kwenye daraja lililojengwa na Mjerumani, hili nakwenda kukaa na mbunge wenu na waziri kuona namna ya aidha kulijenga upya au kulikarabati ili lisilete mafuriko.

“Niwaombe muweke ulinzi na usalama katika maeneo yenu, sababu mkitulia namna hii viongozi tunafikiria namna ya kuwaletea maendeleo lakini mkileta machafuko tunafikiria namna ya kuwakabili. Tukitulia hivi maendeleo yanakuja haraka haraka.

“Tunakuja na mpango wa kurasimisha kutoka kwenye umachinga na kuhitimu kuwa wafanyabiashara wadogo wadogo, kule nako mtachangia kidogo ili maendeleo yaje haraka na changamoto zote zitakwenda haraka,” Rais Samia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad