Jovenel Moise, aliyekuwa rais wa Haiti, ambaye ameuawa juma hili, picha hii ilipigwa mwaka 2018
Jovenel Moise, aliyekuwa rais wa Haiti, ambaye ameuawa juma hili, picha hii ilipigwa mwaka 2018 REUTERS/Jeanty Junior Augustin
Rais wa Haiti, Jovenel Moise, ameuawa akiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia siku ya Jumatano na watu waliokuwa na silaha ambao hawajafahalika hadi sasa, amethibitisha waziri mkuu wa mpito, Claude Joseph.
Katika taarifa yake, waziri mkuu, Joseph, amesema kwa sasa yeye ndio kiongozi wa nchi.
Taarifa zinasema mke wa Moise, alijeruhiwa katika shambulio hilo na anaendelea kupata matibabu, waziri mkuu Joseph, akiwataka wananchi kuwa watulivu wakati huu waliohusika wakisakwa na polisi.
Joseph amesema ''Rais aliuawa akiwa nyumbani kwake na wapiganaji wanaodaiwa walikuwa wakizungumza lugha ya kingereza na Kihispania".
Moise amekuwa akiliongoza taifa hilo masikini zaidi kwenye ukanda wa Amerika kwa amri, baada ya uchaguzi wa wabunge uliokuwa ufanyike mwaka 2018 kuahirishwa kutokana na kutokea sintofahamu ya kisiasa ikiwemo utata kuhusu kukamilika kwa muhula wake madarakani.
Mbali na mzozo wa kisiasa kwenye taifa hilo, vitendo vya utekaji vimeongezeka kwenye taifa hilo pamoja na makundi ya majambazi.
Tangu kukumbwa na Tsunami, taifa la Haiti limeshuhudia hali ya umasikini mkubwa tangu wakati huo.
Moise amekuwa akikabiliwa na maandamano ya kumtaka angatuke madarakani, wapinzani wake wakidai muhula wake ulitamatika, lakini mara zote amekuwa akitumia nguvu kutawala taifa hilo.
Katiba ya sasa ambayo iliundwa mwaka 1987 baada ya kuangushwa kwa utawala wa kiimla wa Duvalier, ilitamka kuwa mabadiliko yoyote yanayolenga kurekebisha katiba kupitia kura ya maoni ni batili, kigezo ambacho rais Moise amekuwa akikitumia ili kutawala.