Rayvanny, Paula Wala Kiapo Cha Kifo



SUPASTAA wa Bongo Fleva, Raymond Mwakyusa au Rayvanny na mpenzi wake mpya, Paula Paul au Paula Kajala, hawapoi; kila kukicha wana jambo na safari hii habari za ndani zimeeleza kwamba, wamekula kiapo cha kupendana hadi kifo kiwatenganishe, IJUMAA limeelezwa.


Mbali na kusema waziwazi kuwa, wanapendana na kuoneshana kwa kuvaa nguo saresare, siri imevuja juu ya wawili hao kujipa majina ya Bonnie na Clyde.

 

Kitendo cha kujiita majina hayo kimeibua kisa cha miaka mingi iliyopita cha kusisimua cha wapenzi, Bonnie (binti mrembo) na Clyde (kijana ‘handsome’) ambao walipendana hadi walipouawa kwa pamoja wakiwa na umri mdogo na majina yao yameendelea kuandikwa, kutamkwa na kutazamwa.

 

Hicho ndicho wanachokitamani Rayvanny au Chui na Paula ambao wameapa kupendana hadi wafe pamoja kama Bonnie na Clyde.



Kupitia Gazeti la IJUMAA unapata kufahamu kwamba, Bonnie na Clyde ni kisa cha kihistoria cha kusisimua mno kuhusu penzi lao, walivyoshirikiana katika matukio ya uhalifu kisha wakauawa pamoja.

 

Historia hiyo ndiyo huwafanya wanamuziki mbalimbali kuwaimba kama Tupac Shakur katika wimbo wake Me And My Girlfriend, Jay Z aliurudia wimbo huo wa Tupac akimshirikisha girlfriend wake wakati huo ambaye sasa ni mkewe, Beyonce Knowles.



Mwaka 1967, wakali wa Pop na Jazz kutoka Ufaransa, Serge Gainsbourg na Brigitte Bardot, walitoa Wimbo wa Bonnie And Clyde, wakiimba kuyafananisha mapenzi yao kama Bonnie na Clyde.Mwaka huohuo, mwanamuziki Georgie Fame alitoa wimbo unaitwa The Ballard of Bonnie And Clyde.

 

Mwaka 1968 mwanamuziki Mel Tamel alitoa Wimbo wa A Day in the Life of Bonnie and Clyde na wengine wengi.Bonnie na Clyde wapo pia kwenye Sinema za Hollywood. Mwaka 1958 iliachiwa Sinema ya The Bonnie Parker Story na mwaka 1976, Arthur Penn aliongoza sinema inayoitwa Bonnie And Clyde.

 

BONNIE NA CLYDE NI NANI?
Nyimbo zimeimbwa, sinema zimetengenezwa, vitabu vimeandikwa kuhusu Bonnie na Clyde, je, watu hao ni akina nani? Maisha yao yalikuwaje mpaka iwe ni historia ya kusimuliwa na vizazi vyote?Bonnie na Clyde walikuwa vijana wapenzi, wenye roho mbaya, katili kwelikweli, lakini walipendana mno hadi walipouawa.



Ni Bonnie Parker na Clyde Barrow. Walipanga mipango mingi ya uhalifu na kutengeneza pesa nyingi ambazo ziliwawezesha kuishi maisha ya starehe.Bonnie na Clyde wanatajwa kwa ukinara wa uhalifu, lakini wakioneshana mapenzi ya dhati.


STORI YA BONNIE NA CLYDE
Mapenzi ya Bonnie na Clyde ni uhusiano ambao haukuwa na usaliti kwani walipendana bila unafiki.Bonnie ashikwe na kiranga mpaka amsaliti Clyde? Angekuwa anajitaka? Clyde ajifanye kupapatikia warembo, halafu Bonnie ajue? Angeponea wapi?

 

Wote hawakuwa na simile lilipokuja suala la kutoa uhai wa mtu.Hofu hiyo ilisababisha Bonnie na Clyde wasisalitiane na hakuna alichpanga mmoja na kutekeleza bila mwenzake kujua.Bonnie na Clyde walipanga pamoja na kutekeleza uharamia wao pamoja.

 

Walitembea pamoja, ilipotakiwa kujificha, walijificha pamoja. Walipofanikisha mipango yao ya uhalifu na kutengeneza pesa, walikwenda kujirusha pamoja.

 

Mahali popote ungemkuta Bonnie, ungezungusha macho ungemwona Clyde. Ungekutana na Clyde njiani, ungetazama vizuri ungemwona Bonnie. Hawakupeana nafasi. Walikuwa na mapenzi ya kugandana kama ruba au kumbikumbi.Kilevi alichotumia Bonnie na Clyde alitumia. Waliishi kwa tafsiri kamili ya jozi (pea).


Kila baada ya kufanikisha mipango yao ya uhalifu hakuna ambacho Bonnie alikihitaji zaidi ya kula maisha akiwa jirani na mwanaume wa maisha yake, Clyde. Vivyo hivyo kwa Clyde dhidi ya mwanamke wa maisha yake, Bonnie.

Mapenzi ya Bonnie na Clyde hayakuwa na kuambiana; ‘I Miss You’, maana hakuna nukta ilipita wakiwa mbalimbali.

 

Kama shughuli za Bonnie na Clyde zingekuwa za halali, basi wangekuwa mfano bora zaidi kwa wapendanao kutokana na ushirikiano wao kikazi na mapenzi yenye nguvu. Tatizo Bonnie na Clyde mapenzi yao yalidumishwa na uhalifu.

 

Bonnie na Clyde walipenda maisha ya juu kwa njia ya mkato na kwa vile walishirikiana ilibidi wagandane kwa kufichiana siri na kulindana. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kuwa na mfano wa kipekee katika mapenzi.Kuna wakati Bonnie alikamatwa kwa mauaji, lakini alikaa miezi miwili jela kabla ya kuachiwa huku Clyde naye akisakwa kwa tuhuma za mauaji.


TAMATI YA BONNIE NA CLYDE
Bonnie na Clyde walidaiwa kuvamia Gereza la Eastham ambalo Clyde aliwahi kufungwa na kutorosha wafungwa ambao walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha ili kuongeza nguvu.Clyde alijua watu wabaya ni akina nani ambao wangeweza kusaidia kuimarisha kundi lao.

 

Ilikuwa Januari 1934, walifanikiwa kuwatorosha wafungwa wengi.Mwanahistoria John Phillips ambaye ni msimuliaji mzuri wa kisa cha Bonnie na Clyde alisema kuwa, tukio hilo ni mafanikio ya Clyde kulipa kisasi dhidi ya Idara ya Magereza ya Texas kwa kumfunga mwaka 1930.

 

Idara ya Magereza ya Texas, iliamua kumshawishi mlenga shabaha maarufu, Frank Hamer na kumpa kazi ya kuwafuatilia Bonnie na Clyde na kuwaua.

 

Vilevile Mkuu wa Idara ya Magereza ya Texas, Lee Simmons, aliwapa kazi walenga shabaha wengine wawili kwa ajili ya kazi hiyo.Waliwafuatilia Bonnie na Clyde hadi siku ile ya Aprili Mosi, 1934; Jumapili ya Pasaka ambapo waliua vijana wawili wauza mafuta.

 

Hali ilikuwa mbaya, Mamlaka za Usalama za Texas na Marekani yote, ziliamka na kutoa tangazo la zawadi nono kwa atakayefichua siri kuhusu mahali walipo.Nyumba zote za starehe, hoteli, baa na kadhalika, Polisi waliwekwa ili kupambana nao. Majina ya Bonnie na Clyde yalitangazwa kila kona.

 

Hali ilikuwa ya wasiwasi, kwani nao kadiri walivyosakwa ndivyo walivyoua na kupora.Mwanahistoria James Knight anasema kuwa, kipindi hicho cha machafuko, Bonnie alionekana mkomavu wa kutumia bunduki, akishambulia sawasawa na Clyde.


SIKU YA KIFO
Kuanzia Februari 12, 1934, walianza kufuatiliwa hatua kwa hatua huko Texas hadi siku ile ya Mei 21, 1934, walipogundulika kuwa siku hiyo walikuwa na safari ya kwenda Parokia ya Bienville, Lousiana.Mei 23, 1934, saa 3:15 asubuhi, Bonnie na Clyde walikuwa kwenye gari aina ya Ford V8 Fordor Delux Sedan toleo la mwaka 1934.

 

Clyde akiwa ndiye anaendesha, alimkuta njiani baba yake, Methvin, alipoanza kuzungumza naye, Polisi wanne, wataalam wa shabaha walimshambulia Clyde na kumuua hapohapo.Baada ya hapo walimgeukia Bonnie aliyekuwa kwenye gari, siti ya abiria na kumwagia risasi kisha naye akafa. Hadithi ya Bonnie na Clyde ikaishia hapo.


RAYVANNY NA PAULA
Achana na suala la uhalifu kwa sababu hawatafika popote, lakini chukua kipengele cha kupendana kwa dhati hadi kifo kitakapowatenganisha kwani hicho ndicho walichoapa kukifanya Rayvanny na Paula.

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad