Baada ya kuifunga Kaizer Chief magoli 3-0 kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika usiku wa Julai 17, 2021, klabu ya Al Ahly imetwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo.
Mbali na kutwaa mara mbili mfululizo lakini miamba hiyo ya soka kutoka nchini Misri imeendelea kutanua wigo wa rekodi yake ya kuwa mabingwa wa kihistoria wa kombe hilo ambapo sasa wamefikisha mara 10.
Kwa upande wa kocha wa timu hiyo Pitso Mosimane ametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu. Alitwaa ubingwa wake wa kwanza msimu wa 2015/16 akiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kisha msimu wa 2019/20 akiwa na Al Ahly na sasa 2020/21 akiwa bado na Al Ahly.
Kaizer Chiefs ambao walikuwa wanacheza fainali yao ya kwanza katika historia yao, walifika hatua wakiacha kumbukumbu ya kuitoa Simba SC ya Tanzania katika hatua ya robo fainali kabla ya kuitoa Wydad Casablanca kwenye nusu fainali.