Arusha. Mkuu wa shule ya Sekondari ya Kisirimi amesema kuongoza matokeo ya kidato cha sita mwaka wa tatu mfululizo sio uchawi bali ni mipango, mikakati, utekelezaji mikakati na usimamizi mahiri.
Akizungumza na mwananchi leo Julai 10, Mkuu wa shule hiyo, Valentine Tarimo amesema mambo hayo manne wamekuwa wakiyasimamia na matokeo yake yamekuwa ni kupata matokeo bora kila mwaka.
Amesema ili kufikia malengo hayo, shule hiyo imekuwa na mikakati inayoshirikisha walimu wote, wanafunzi, wazazi, serikali na majirani wa shule hiyo.
"Tumekuwa tukikaa pamoja na kuweka malengo ya kufanya vizuri na kuhakikisha wote tunakuwa na lengo moja, wanafunzi kusoma, walimu kufundisha pamoja na wazazi na majirani wa shule kutoa ushirikiano ambao unahitajika," amesema Tarimo.
Tarimo anasema mwaka 2019 shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza baada wanafunzi 52 kupata daraja la kwanza na wawili daraja la pili, huku mwaka 2020 wanafunzi wote 62 wakipata daraja la kwanza na mwaka huu wanafunzi wote 72 wamepata daraja la kwanza.
Shule hiyo ya kata ilianzishwa mwaka 2002 kwa madarasa ya hadi kidato cha nne na baadaye mwaka 2006, kuanzishwa kidato cha tano.