Samia awataka Watanzania wavumilie kamati ya kutathmini tozo




Rais Samia Suluhu amesema tozo za miamala ya simu zipo palepale lakini Serikali inakwenda kuangalia njia ya kulitekeleza, akiwataka Watanzania wasubiri matokeo ya kamati iliyoundwa kutathmini malalamiko ya suala hilo.


Rais Samia amesema hayo Julai 27 mara baada ya kuwaapisha mabalozi wapya 23 Ikulu ya Dar es Salaam, akisema baada ya kuanza kwa tozo kelele zilikuwa nyingi, Serikali ilisikia na kuunda kamati.



“Makato haya tuliyaweka kwa nia njema tu, nchi yetu sasa hivi wakulima wameamka na kilimo kikubwa lakini wakivuna wanashindwa kutoa mazao yaliko kuleta kwenye maeneo ya masoko, tatizo ni njia za vijijini hakuna, kwa hiyo sehemu kubwa ya fedha hizo inakwenda kujenga njia za vijijini,” amesema Rais Samia.



Vilevile amesema maeneo mengi yana changamoto ya maji kwakuwa asilimia 26 bado haijafikiwa, fedha hizo pia zinakusudiwa kupelekwa kwenye miradi ya maji.



“Niwaambie Watanzania tumesikia vilio, tunakwenda kuangalia njia nzuri ya kwenda na hili lakini hizi tozo nataka niseme zipo, ila tutaangalia njia nzuri ambayo haitaumiza watu, serikali ipate na maendeleo yaendelee, Kazi iendelee,” alisema.



Kuhusu kupande bei kwa bei ya mbolea amesema hilo limesababishwa na viwanda vya mbolea vya nje kutozalisha kwa muda mrefu kwasababu ya kufungwa baada ya mlipuko wa Covid-19 na hata kazi kubwa za mashambani zilikuwa hzifanyiki.



Amesema Serikali inalijua hilo na imeshachukua hatua za makusudi ili kuhakikisha mbolea inapatikana ndani ya nchi na kwa bei ambayo wakulima wataweza kumudu.



“Moja kati ya hatua kuna kiwanda kikubwa cha mbolea kinajengwa Dodoma tutahakikisha tunaotoa msukumo wote ili kizalishe kwa haraka ili msimu unaofuata mbolea itoke hapa hapa nchini,”alisema Rais Samia.



Aidha Rais Samia ametoa wito kwa mabalozi hao wapya ambao ni wa kwanza kuteuliwa tangu alipoingia madarakani, kuhakikisha kuwa wanaimarisha na kukuza uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine kuibua fursa za kiuchumi, kiafya na kielimu katika maeneo waliyopo ambazo zinawafaa watanzania

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad