Serikali yatoa siku 14 tozo mpya za mitandao



Dar/Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ametoa siku 14 kuanzia jana hadi Julai 15 kwa watoa huduma wote wa mitandao ya simu kurekebisha mifumo yao na kuanza kutoza makato mapya ya Serikali.

Pia, Serikali imewataka wateja wanaotumia simu za mkononi kuhakiki namba yao ya kitambulisho cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kama imetumika kusajili laini za simu ambazo mmiliki wa kitambulisho hazijui.

Mwezi uliopita Bunge lilipitisha tozo ya kuanzia Sh10 hadi Sh10,000 itakayotozwa katika kila muamala wa kutuma au kupokea fedha na kiwango kati ya Sh10 hadi Sh200 kwa siku kila mteja anapoongeza salio la muda wa maongezi kwenye simu.

Dk Nchemba alisema hatua hiyo itasaidia Serikali kuanza kukusanya fedha hizo zitakazotumika kuboresha miundombinu na miradi ya maendeleo mbalimbali ili kuwakwamua wananchi wanaopata adha.

Alisema Serikali imepanga kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ya wananchi na inayohitaji fedha nyingi na jukumu la kukamilisha mchakato huo ni la Watanzania wote wenye uchungu wa maendeleo.

“Fedha zitakazopatikana kwenye tozo hizo hazitatumika kulipa mishahara wala kugharamia matumizi mengine ya Serikali, bali zitapelekwa moja kwa moja kutatua changamoto za afya na elimu.

“Zitaboresha miundombinu ya barabara, miradi ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa na bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere,” alisema Dk Nchemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na wizara hiyo, Dk Nchemba alisema hayo wakati akizungumza na Chama cha Watoa Huduma wa Simu Tanzania (Tamnoa), kuwa kodi ya miamala ya simu na vifurushi vya mitandao vitakavyotozwa, inalenga kila Mtanzania kuchangia mapato ya Serikali.

Dk Nchemba alisema jambo la kutia moyo ni kuwa Watanzania wameunga mkono kutozwa kodi hiyo, kwa kutambua umuhimu wa maendeleo yao ambayo kukamilika kwake kunahitaji mchango wao.

“Kampuni za simu msichukulie makato haya kama kodi nyingine mnazowatoza wateja wenu. Bali Serikali iliamua kuweka makato haya kwenye miamala ya kuweka muda wa maongezi na kufanya miamala kwa njia ya simu ili watumiaji wengine wa simu wachangie maendeleo ya nchi,” alisema Dk Nchemba.

Akizungumza kwa niaba ya Tamnoa, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Vodacom, Roselynn Mworia alisema wamepokea mpango huo kwa mikono miwili na kuwataka wateja wao kuiunga mkono Serikali, huku akiomba iwape muda wa kurekebisha mifumo yao kwa kuwa mchakato huo unahitaji muda wa kiufundi.

Kuhusu uhakiki wa usajili, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustin Ndugulile aliwataka wananchi kuhakiki namba zao za Nida kwa kubonyeza *106# kama hazijatumika kusajili laini nyingine za simu ili kukabiliana na wimbi la uhalifu wa kimtandao

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad