Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Katiba ya Tanzania ni nzuri, inapaswa kuheshimiwa kwa kuwa imeivusha nchi katika kipindi kigumu.
Alisema uzuri wa Katiba na umadhubuti wake huonekana wakati wa matatizo yasiyo ya kawaida, hivyo inafaa kuheshimiwa.
Profesa Kabudi alisema mabadiliko mengi ya Katiba yalifanyika mwaka 1984, hivyo ni vyema kuendelea kuienzi kwa sasa wakati utaratibu mwingine unasubiriwa.
Kauli hiyo inakuja zikiwa zimepita takribani siku tatu tangu viongozi wa dini nchini kueleza umuhimu wa Katiba Mpya, huku Chadema kupitia kongamano maalumu lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha), likieleza umuhimu wa suala hilo juzi.
Profesa Kabudi alitoa kauli hiyo jana katika maadhimisho ya saba ya siku ya utetezi wa haki za binadamu, yaliyofanywa na asasi za kiraia nchini pamoja na uzinduzi wa utekelezaji wa mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano wa azaki hizo.
Alisema baada ya Rais John Magufuli kufariki dunia, makamu wake (Rais Samia Suluhu Hassan) aliapishwa kushika wadhifa huo kwa matakwa ya Katiba kupitia Ibara ya 9 na sasa nchi ina Rais mtendaji mwanamke na mwenye uwezo.
“Hili lilikuwepo ndani ya Katiba, limeivusha nchi yetu katika kipindi hiki kigumu na uzuri wa Katiba na umadhubuti wake unauona wakati wa matatizo yasiyokuwa ya kawaida. Tanzania imevuka mtihani huo kwa katiba hii na tumshukuru sana Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kutuwekea misingi ambayo imetufikisha hapa, nchi nyingine za Afrika kwa hili lililotokea ni vita, dhahama na migogoro, sisi salama salimini, Samia Suluhu Hassan amepokewa vizuri na raia wote wa Jamhuri ya Muungano bila maswali,” alisema Profesa Kabudi.
Pia, alisema mbali na hayo, Katiba ya sasa imekuwa msaada mkubwa kiutendaji na inalinda haki za binadamu na utawala bora.
“(Katiba ya sasa) Inalinda haki za kiraia, kisiasa, uchumi na za kiutamaduni na ndiyo maana Serikali imeridhia kwanza Katiba yetu,” alisema.
Katika kongamano la Bavicha, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitaka Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya Katiba ili kusimamia mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Mbowe alisema Watanzania wanahitaji Katiba Mpya, bora na shirikishi, huku akipendekeza makundi mbalimbali ya kijamii yashirikishwe.
Alisema hatua ya pili iwe ni kuunda Bunge Maalumu la Katiba litakalozingatia masilahi ya makundi yote.
Awali, akizindua mkutano huo, Profesa Kabudi alizitaka asasi hizo za kiraia kuacha kutegemea wahisani, bali wajitegemee kutafuta vitu vya kuwaingizia kipato pamoja na kufuata sheria za nchi wanapofanya kazi zao.
“Wakati umefika asasi za kiraia kuanza kufikiria kutafuta njia nyingine za kuziwezesha asasi hizi kifedha kuliko kuendelea kusaidiwa, siwezi kusema tuache kusaidiwa, ila tuanze kufikiria kwenda mbali,” alisema Profesa Kabudi.
“Asasi nyingi bado zinajikita katika dhana ya Serikali kama mvunjifu mkuu wa haki za binadamu na matokeo yake hazielekezi nguvu kubwa katika kupambana na uvunjifu wa haki za binadamu unaofanywa na raia au kampuni na mashirika makubwa ya kiuchumi duniani.”