Barakoa ni kifaa tiba kinachovaliwa na kufunika eneo la pua na mdomo kwa lengo ya kuzuia au kupunguza vijidudu vya maradhi, hewa chafu na maji maji kutoka kwenye mazingira kwenda kwa mtumiaji.
Baada ya nchi kukumbwa na wimbi la tatu la Covid-19, uvaaji barakoa umerudi kwa lengo la kujikinga na maradhi hayo, lakini swali la kujiuliza ni kwamba, barakoa unayovaa ina ubora?
Mtaalamu wa elimu kwa umma kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Amma Kasangala alitegua kitendawili hicho akisema barakoa inayotakiwa kuvaliwa ni ile iliyotengenezwa kwa kutumia malighafi za pamba kwa asilimia 100.
Alisema barakoa hiyo lazima iwe na kitambaa zaidi ya kimoja na ifunike vizuri maeneo yaliyolengwa.
“Lazima iwe pamba, kwa asilimia 100 halafu iwe na leya zaidi ya moja, hii ni ile inayotumika na kufuliwa yaani barakoa ya kushona. Inatakiwa kuziba vizuri pua na kufunika kidevu,” alisema Dk Kasangala.
Pia, alisema kumekuwa na barakoa zinazoshonwa ambazo ni ndogo, hivyo huteremka wakati wote.
“Hizi hazitakiwi kwa kuwa uwezekano wa kumkinga mvaaji wakati wote unakuwa mgumu.”
Alipoulizwa kuhusu barakoa ambazo hazijatengenezwa kwa malighafi za pamba zilizoenea kwa wafanyabiashara wengi alisema, “barakoa zisizotengenezwa kwa malighafi ya pamba sio sahihi, zipo zinauzwa maeneo mengi na nyingine zina vitundu, hizi zote hazina viwango kwa kuwa haziwezi kumkinga mhusika dhidi ya virusi vya corona.”
Alizitaja barakoa nyingine za kutengeneza viwandani ‘surgical mask’ kwamba hazina tatizo kwa kuwa zina viwango sawa na zile zinazotumika na wataalamu wa afya, zikiwamo N95.
Hata hivyo, Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania (TMDA) imeandaa mwongozo unaoelekeza matakwa muhimu ya barakoa pamoja na watengenezaji wake.
Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma TMDA, Gaudensia Simwanza alisema wameidhinisha vigezo vya barakoa za vitambaa kwa ajili ya matumizi ya kawaida lakini zinatakiwa kukidhi vigezo.
“Zitengenezwe kwa kutumia vitambaa visafi, zimtoshe mvaaji vizuri eneo lote la pua, mdomo na kidevu bila kulegea,” alisema Simwanza.
Pia, alisema barakoa lazima ziwe na vifungio, kamba au mpira laini kama vishikizio masikioni na kuwe na kitambaa zaidi ya kimoja, yaani kitambaa cha ndani na kitambaa cha nje na ikiwezekana kitambaa cha kati.