BAADA ya kumalizana na kipa wa Tanzania Prisons, Jeremiah Kisubi, inaelezwa kuwa uongozi wa Klabu ya Simba umemficha kipa huyo Dar es Salaam.
Wakati akiwa amefichwa Dar, klabu yake ya Prisons inafahamu kipa huyo anashughulikia matatizo ya kifamilia kama ambavyo ruhusa yake inavyosema.Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinaeleza kuwa tayari Kisubi amefikia makubaliano mazuri na klabu hiyo na kusaini mkataba wa miaka mitatu.
Anajiunga na timu hiyo akiwa kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na Prisons kumalizika mwisho wa msimu huu.Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Kikosi cha Prisons, Prosper Mtevu, alisema: “Ni kweli kipa wetu Jeremiah Kisubi hayupo na timu tangu Juni 18, mwaka huu kutokana na ruhusa maalum ambayo alipewa ya kwenda kushughulikia matatizo ya kifamilia.
“Kuhusiana na ishu ya kusaini Simba, inawezekana akawa tayari amesaini au sivyo kwa kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, kiutaratibu ana nafasi ya kusaini kwenye timu nyingine kama mchezaji huru, hivyo tutasubiri kuthibitisha hilo atakapokuja kutuaga.”
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu kuzungumzia ishu hiyo, alisema: “Ni kweli kama uongozi malengo yetu ni kuhakikisha tunazidi kuwa bora kwa kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango bora.
“Lakini siwezi kusema chochote kuhusiana na mipango ya usajili kwa sasa kwa kuwa bado tunasubiri ripoti ya kocha kufahamu mapungufu yapo wapi ya kuyafanyia kazi, hivyo kuhusiana na hilo tunaomba muda zaidi wa kulifanyia kazi kabla hatujatoa taarifa rasmi.”JOEL THOMAS, Dar es Salaam