Th. 570 Bilioni Kunufaisha Wanafunzi 160,000 Mikopo Elimu Ya Juu



Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepanga kutumia bajeti ya kiasi cha TZS 570 Bilioni katika mwaka 2021/2022 inayotarajia kuwanufaisha zaidi ya wanafunzi 160,000.


Akizungumza jana (Ijumaa, Julai 2, 2021) jijini Dar es salaam katika hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kiwango cha fedha kilichotengwa kwa 2021/2022 kimevunja rekodi katika miaka 16 ya uhai wa HESLB.


Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako, kati ya wanafunzi hao 160,000, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatarajiwa kuwa 62,000 wakati wanaoendelea na masomo watakua 98,000.


“Niwaibie siri tu. Hadi mwezi uliopita, bajeti ya mikopo kwa mwaka 2021/2022 ilikua TZS 500 bilioni. Lakini katika siku zake 100 za uongozi kama Rais wetu, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ameongeza TZS. 70 bilioni na kufikia hizi TZS. 570 bilioni kwa mwaka 2021/2022 sawa sawa na ongezeko la TZS. 106 bilioni (22.8%)” alisema Prof. Ndalichako.


Aliongeza kuwa ongezeko hilo linathibitisha nia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuwawezesha vijana wengi kupata fedha na kusoma ili watumikie nchi yao na kuwataka waombaji wahitaji watulie, na kusoma maelekezo na kuomba kwa usahihi ili watimize ndoto zao.


Katika mwaka wa masomo wa 2020/2021, Serikali imetenga na kutoa TZS 464 bilioni zinazowanufaisha jumla ya wanafunzi 149,398. Kati yao, wanafunzi 55,287 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 94,111 ni wale wanaoendelea na masomo.


Aidha katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako aliitaka HESLB kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa waombaji ili waweze kuelewa sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa usahihi na kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwasaidia vijana wengi wanaoomba mikopo.


Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema wamepokea maelekezo na kuanzia Julai 12 mwaka huu, maafisa wa HESLB wataanza kuendesha programu za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi chini ya kampeni ya #WeweNdoFuture.


“Tunakamilisha utaratibu na uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili tuwafikie vijana wote waliopo katika kambi 19 za JKT kuanzia Julai 12 … tutaendesha pia programu hizi kupitia televisheni, redio, mitandao ya kijamii na mikutano na wadau,” amesema Badru.


Kuhusu utaratibu na muda wa kuomba, Badru amesema Mwongozo wa Uombaji mkopo unaoeleza sifa na utaratibu wa kuomba mkopo unapatikana katika www.heslb.go.tz kuanzia leo (Ijumaa, Julai 2, 2021).


“Mwongozo upo katika tovuti kuanzia leo, Julai 2 na tunawashauri waombaji wausome kabla ya kuomba. Aidha, mfumo wa kupokea maombi kuwa wazi kwa siku 53 kuanzia, Julai 9 hadi Agosti 31, 2021,” amesema Badru.


Mkutano huo wa uzinduzi pia uliohudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe na wawakilishi kutoka Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao pia huwahudumia waombaji mikopo.


HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria, ikiwa na majukumu makuu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali kwa wanafunzi wa elimu ya juu tangu mwaka 1994/1995.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad