MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema chama hicho kikitengeneza utaratibu wa kufanya mikutano ya hadhara kwa ajili ya kudai katiba mpya, atarejea nchini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Lissu ametoa kauli hiyo jana Alhamisi, tarehe 1 Julai 2021, akizungumza kwa njia ya mtandao, katika uzinduzi wa kongamano la kudai katiba mpya, lililofanyika kwenye ukumbi wa Baracuda, Tabata jijini Dar es Salaam.
Mwanaaiasa huyo aliyeko nchini Ubelgiji amesema, chama hicho kikitaka katiba mpya ipatikane, lazima kishirikishe wananchi.
“Tuwaandae wananchi kwenye mikutano ya hadhara na mimi niwaahidi, tukitengeneza utaratibu wa mikutano ya hadhara, nakuja Tanzania. Nitakuja Tanzania kufanya mikutano ya hadhara, sio kuja kujifungia chumbani na kukaa kwenye vikao vya ndani. Tujiandae kwenda kwa wananchi tutapata katiba mpya,” amesema Lissu.
Awali, akizindua kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, aliwaagiza viongozi wa chama hicho wajiandae kufanya mikutano ya siasa.
“Kwanza tuna amani mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni haki ya kikatiba kisheria na ni wajibu wetu, ombi la mama Samia kwamba tusubiri, tumpe muda hatuko tayari kumpa muda.
Hatuko tayari kumpa Mama Samia muda, na natoa agizo kwa viongozi wote wa chama nchi nzima wajiandae mapema kwa ajili ya mikutano ya hadhara, siku ambsyo tutaitangaza,” alisema Mbowe.
Wakati huo huo, Lissu amekishauri chama hicho, kihoji makundi mbalimbali juu ya misimamo yake kuhusu upatikanaji katiba mpya.
“Sasa tunajiandaaje, Rais Samia alikutana na maaskofu juzi juzi, tuwaombe maaskofu na sisi tukutane nao tuwaambie wachague upande, tujue kama wanataka upande wa katiba ya wananchi. tuwaendee Mashekhe wetu tuwaambie wachague upande, tuendelee na utawala huu au wanataka katiba mpya,” amesema Lissu.
Mwanasiasa huyo ameongeza”tuendelee kwa taasisi zote tuwaambie wachague upande, wanachagua utawala uliopo au wanaunga mkono katiba ya wananchi. tusiwe na watu tusiojua misimamo yake.”