Dar es Salaam. Marekani imesema ndege ya jeshi la nchi hiyo iliyoegeshwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) imeleta mahitaji muhimu ya ubalozi wa nchi hiyo nchini Tanzania.
Ndege hiyo ambayo kwenye bawa lake la nyuma ina bendera ya Marekani chini yake ikiandikwa herufi AMC, picha zake zilianza kusambaa mitandaoni kuanzia jana Alhamisi Julai Mosi, 2021 ikiwa katika uwanja huo uliopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Julai 2, 2021 ofisa ubalozi wa Marekani,
Michael Pryor amesema, “ni kweli ni ndege ya Marekani. Huwa inakuja kila mwaka kwa nyakati tofauti kushusha mahitaji muhimu ya ubalozi wa Marekani hapa nchini na kwingineko jirani.”
Bila kuyataja mahitaji hayo Pryor amesema huenda ndege hiyo ikaondoka kesho baada ya kukamilisha ushushaji. Katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu walihoji ujio wa ndege hiyo bila majibu na wengine walijibizana kuwa huenda imeleta chanjo za Covid-19 baada ya Serikali kuruhusu uingizaji wa chanjo hizo kwa jumuiya za kimataifa.