Mwanza. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza limesema tukio la wafanyakazi wanne wa kampuni ya kubeba makontena ya Khimji limetokea baada ya winchi iliyokuwa inahamisha kontena ya mfanyabiashara kugusa nyaya za laini kuu ya umeme.
Wafanyakazi hao wamejeruhiwa na shoti ya umeme wakati wakibomoa vibanda vya wafanyabiashara wadogo katika mtaa wa Kirumba kati leo Alhamisi Julai Mosi, 2021 kwa amri ya baraza la ardhi na makazi Mkoa wa Mwanza lililowataka kuondoka katika eneo hilo kuanzia Juni 5, 2021.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Julai Mosi, 2021 Kaimu Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Kamo amesema wahusika wamejeruhiwa kirahisi kwa kuwa hawakuvaa vikinga mwili.
"Baada ya maofisa wetu kuwasili katika eneo lilipotokea tukio tumebaini majeruhi hao wanne hawakuwa wamevaa mavazi yanayoweza kuwakinga na ajali hasa za moto wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao," amesema Kamo.
Mwananchi Digital imefanikiwa kufika katika hospitali ya Royal walipopelekwa majeruhi hao huku wamiliki wa kampuni ya Khimji wakishugulikia taratibu za matibabu yao.
Daktari aliyewapokea majeruhi hao katika hospitali ya Royal, Dk Samuel Jackson amewataja kuwa ni Shaaban, Jamal, Ali na Kamugisha na kwamba wamechubuka maeneo mbalimbali mwilini, “pia wamepoteza kumbukumbu kwa muda lakini matibabu yanaendelea kuwarejesha katika hali ya utimamu.”
"Tumewapokea majeruhi wanne na tumewalaza katika hospitali yetu wakati tukiendelea na uchunguzi wa kina kutambua madhara ya ajali hiyo.”