Unaambiwa Madaktari Waingia Hofu Kasi Ugonjwa wa Corona Nchini



Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kusisitiza tahadhari dhidi ya maambukizo ya corona, madaktari wameshauri kuchukuliwa hatua za kuwalazimisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo.

Wataalamu hao wa afya wamesema tangu Jumatatu idadi ya wagonjwa wenye dalili za corona wamekuwa wakiongezeka, hivyo vyombo husika havina budi kuunga mkono juhudi za Rais kupambana na ugonjwa huu.

Rais Samia juzi akiwa Morogoro aliwataka Watanzania kuchukua tahadhari zote, ikiwemo kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko kwa kuwa wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 limeanza kusambaa.

Aliitaja mikoa yenye ongezeko kuwa ni Kagera, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na Dodoma.


RMO ataka hatua za lazima

Wakati hali ikiwa hivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa ameiomba Serikali mkoani humo kufanya tahadhari za kujikinga na virusi vya corona kwa wananchi kuwa za lazima.

Akizungumza katika kikao cha kuweka mikakati ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19 mkoani humo juzi, Dk Rutachunzibwa alisema mwitikio duni wa watu kujikinga na corona imekuwa changamoto ya kudhibiti kuenea kwa maambukizo hayo.

“Miongoni mwa changamoto katika mapambano haya ni mwitikio mdogo wa jamii kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa, hivyo sisi kama wataalamu tukuombe mkuu wa mkoa (Robert Gabriel) uchukuaji huu wa tahadhari uwe wa lazima, maana tusipofanya hivi huenda madhara yakawa makubwa,” alionya Dk Rutachunzibwa.


Maagizo ya Rais yapewe uzito

Akizungumza na Mwananchi jana, mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisema juhudi zinazofanywa na Rais Samia zipokewe kwa uzito uleule na viongozi wa chini, ili kunusuru wananchi na madaktari walio mstari wa mbele kupambana na tatizo hilo.

“Tatizo lipo nchini, kila kunapokuwa na mikusanyiko wagonjwa wanaongezeka, tunashauri watu wavae barakoa na wajikinge pia kwa njia nyingine, ikipendeza kila nyumba iweke maji tiririka na sabuni.

“Kadri mikusanyiko inavyoendelea sisi tunazidi kupokea wagonjwa. Kuanzia Jumatatu tunaona wagonjwa wanazidi kuongezeka, yaani maneno ya Mama yasimamiwe na watendaji wake,” aliongeza Dk Osati.

Msisitizo wa ushauri huo umetolewa na Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe akishauri msukumo wa watu kufuata kanuni za kujikinga uongezeke tofauti na ilivyo hivi sasa.


“Msisitizo uongezeke. Katika vyombo vya usafiri wa umma watu wavae barakoa, iwe ni lazima pia kunawa kwa maji safi tiririka na sabuni na matumizi ya vitakasa mikono, hii itasaidia kupunguza ugonjwa huu kusambaa kwa kasi kama ilivyo hivi sasa,” alisema.

Dk Mwaibambe alishauri Wizara ya Afya ijikite katika matangazo sehemu zenye mikusanyiko ya watu kwa kutumia magari maalumu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kuwahamasisha watu kuvaa barakoa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha watoa huduma za afya Tanzania (Aphta), Dk Samwel Ogilo alisema wananchi bado hawaamini kama ugonjwa huo upo, ingawa ukweli ni kwamba Covid-19 ipo nchini.

Alionya kuwa tahadhari zisipochukuliwa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, nchi itaingia katika hasara kubwa na wananchi watateketea.


“Madhara yatakuwa makubwa, kama tulivyoona katika nchi nyingine jirani,” alionya.

Viwanja vya ndege

Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe amewaagiza watumishi wote wa afya katika mamlaka za viwanja vya ndege kujilinda wenyewe kwa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa corona kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji safi tiririka.

Alisema suala la kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona si tu kwa watumishi peke yao, bali wageni wageni pia wanaotoka na kuingia nchini, huku akisisitiza kuwa pamoja na kuchukua vipimo vya watu, waendelee kuwasisitiza kujikinga, ikiwemo kuvaa barakoa.

Ushauri wa Mbatia

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema hali ya Covid-19 hapa nchini ni mbaya, lakini anashangaa kuona viongozi wa Serikali wakipuuzia hilo na kushindwa kuchukua hatua ambazo zitawafanya wananchi wachukue tahadhari.

Aliitaka Serikali kuanza kutoa takwimu za wagonjwa walio hospitali na waliofariki kwa ugonjwa huo sambamba na kuongeza vituo vya kupima ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali ya nchi ili iwe rahisi kubaini maambukizi.


“Vituo vya kupimia Covid-19 viko wapi? Dar es Salaam nzima yenye watu zaidi ya milioni 5, kituo cha kupimia Covid-19 kiko kimoja tu, Maabara ya Taifa, tuko makini kweli?” alihoji mwanasiasa huyo.

Imeandikwa na Herieth Makwetta, Peter Elias, Mgongo Kaitira na Saada Amir.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad