Arusha. Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita umeuomba upande wa Serikali katika kesi hiyo kumaliza upelelezi kwani washitakiwa wako ndani kwa muda mrefu.
Maombi hayo yametolewa leo Ijumaa Julai 30, 3021 baada ya mawakili wa Serikali kuomba kupangiwa tarehe nyingine ya kesi hiyo.
Katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha, upande wa Serikali uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula na Wakili wa Serikali Baraka Mgaya.
Upande wa utetezi uliwakilishwa na Mawakili Dancan Oola na Mosses Mahuna.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27, 2021 ilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Amalia Mushi.
Wakili Kweka aliieleza mahakama kuwa shauri hilo lilipangwa kwaajili ya kutajwa na kuwa wanaomba tarehe nyingine kwaajili ya kutajwa shauri hilo ambapo alidai upelelezi uko katika hatua za mwisho.
"Kesi leo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa ili kueleza hatua zilizofika katika upelelezi uko katika hatua za mwisho tunaomba tarehe nyingine ya kutaja ili tuweze kuomba amri nyingine ya mahakama,"aliomba
Kwa upande wake Wakili Oola aliieleza mahakama kuwa hawana pingamizi ila wanaomba upelelezi wa suala hilo uweze kukamilika kwani washitakiwa wako ndani muda mrefu.
"Hatuna pingamizi tunaomba upande wa serikali wafanye kinachowezekana kumaliza upelelezi wa suala hili kwa sababu washitakiwa wako ndani kwa muda mrefu sasa,"
Hakimu Amalia aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13, 2021 kwa ajili ya kutajwa.
Katika Kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha ambayo Sabaya na wenzake wawili, wanashitakiwa Kwa makosa matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha.leo imeendelea.
Upande wa utetezi, unaendelea kumuhoji shahidi wa sita Bakari Msangi ambaye alieleza jinsi alivyopigwa na Sabaya na kunyang'anywa fedha na simu .
Katika Kesi hii Sabaya anashitakiwa na walinzi wake Sylivester Nyegu na Daniel Mbura ambao wanadaiwa February 9 mwaka huu katika duka la Mohamed Saad walivamia na kufanya unyang'anyi wa kutumia silaha wa zaidi ya sh 2.7 milioni