JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imelaani na kupinga kauli za Mbunge la Kawe, Josephat Gwajima (CCM) kwamba atakaye ‘shadadia’ suala la chanjo bila kufanya utafiti wa kina kujua madhara ya muda mrefu na mfupi atakufa.
UVCCM imeiomba (CCM) kumchukulia hatua kali za kinidhamu huku kikidai Gwajima atambue anaetoa na kuchukua uhai ni Mungu na hakuna Mkristo zaidi ya Papa Francis ambaye ametoa ‘Walaka’ watu wajikinge na ugonjwa wa corona.
Mchungaji na Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima.
Gwajima ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, katika Ibada ya Jumapili wakati akiwahubiria waumini wake alionesha mashaka kuwa chanjo za Uingereza na Tanzania zinaweza kuwa hazifanani.
Akizungumza leo Jumanne Julai 27, na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Sekretariet ya Umoja huo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenan Kihongosi amesema wanalaani na kupinga kauli za mbunge huyo kwani amezungumza matamshi yasiyofaa kwa wananchi kwani Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa msimamo kuhusiana na chanjo.
“Juzi tumeona kuna baadhi ya viongozi wamezungumza matamshi yasiyofaa Mbunge wa Kawe Ndugu Gwajima ameweza kutoa maneno yasiyofaa kwa wananchi na maneno yale ni ya kichochezi na yanaenda kuwagawa wananchi kwa sababu Mheshimiwa Rais na Serikali wameishatoa msimamo kwamba wananchi waweze kupata chanjo.
“Na chanjo imeishaletwa, sasa anapotokea kiongozi mmoja wa mhimili anakwenda anazungumza Kanisani na kuwahubiria waumini ambao na wao wana watu nje kwamba natuma message hiyo chanjo haifai na chanjo hiyo ina madhara.
“Sasa yeye labda tuhoji yeye ni Dakrati amesomea? Amejuaje mambo haya hayafai? Sambamba na hilo ni utovu wa nidhamu kwa sababu msimamo wa serikali ni kulinda watu wake na tumeona chanjo ikitolewa wananchi watapata unafuu wa gonjwa la corona,”amesema Kihongosi.
Amesema UVCCM wanachojua kuna vikao maalum vya kupeleka hoja na sio kukurupuka kama alivyofanya Askofu Gwajima huku wakidai lazima atambue yeye sio mungu na anaetoa na kuuchukua uhai ni Mungu,” amesema Kihongosi.