Waliohujumu fedha NHIF ‘kuzitapika’



 
Waliohujumu fedha NHIF ‘kuzitapika’
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amewataka watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) waliohujumu mfuko huo kwa kujiandikia malipo wasiostahili wajiandae kulipa fedha hizo.

Akizindua Bodi ya NHIF pamoja na kuzindua maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, jijini Dodoma jana, Dk Gwajima alitangaza kiama kwa waliofanya ubadhirifu mfuko huo.

“Shirika pamoja na wizara kwa ujumla imekuwa ikipokea malalamiko ya watoa huduma na makato yanayofanywa, yapo makato mengine si kwa sababu ya makosa ya kujaza fomu vibaya kwa bahati mbaya au makusudi, bali ni ubadhirifu uliotokea katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo,” alieleza.

Alisema upo ubadhirifu kwa watu kughushi nyaraka ili walipwe malipo yasiyo halali. “Wapelekeeni salaamu katika kona zote nchini,” alisema na kuwataka wahusika wakae majumbani mwao wakiwaza namna ya kulipa fedha hizo.


 
“Hao ni wezi na nitoe salaamu wanaofanya ubadhirifu kwenye mfuko huu nitashughulika nao. Ripoti ipo mwenyekiti ichukue, atenge kabisa fungu naanza utaratibu kuzichukua naanza utaratibu wa kuzirudisha, mwekeeni mpango wa kuzilipa,” alisema Dk Gwajima na kuwaomba wote wenye taarifa za ubadhirifu huo wampatie.

Alizungumzia pia utendaji katika vituo vya afya vya serikali akisema kuna uwajibikaji mbovu kulinganisha na zile binafsi. Pia alizungumzia suala la ukopaji fedha za kutolea huduma.

“Hili ni tatizo, hawataki kwa kukopa, hata kama mfuko umetenga shilingi bilioni 12 na zinatumika bilioni mbili, huku waananchi wanapofika katika vituo hivyo, wanakosa dawa, vifaa tiba na uboreshaji,” alieleza.


Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel alisema wanaandaa utaratibu wa kujua ni madaktari wangapi wanafanya kazi za nje au kwenda kutibu katika hospitali binafsi wakati wa muda wa serikali.

“Mfumo huo utasaidia kujua daktari gani ametibu wapi na wakati gani, wakati mwisho wa siku anataka kulipwa na serikali kumbe amekwenda kutibu katika hospitali binafsi,” alieleza.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa NIHF, Bernard Konga alisema tangu mfuko uanze Julai Mosi, 2001, kuna wanufaika milioni 4.3 ambao ni sawa na asilimia nane ya Watanzania, wakati mifuko ya bima kwa ujumla wake inahudumia asilimia 14 ya Watanzania.

Konga alisema mfuko huo umesonga mbele katika masuala ya utumiaji wa tehama ambapo sasa imefikia asilimia 90 ya shughuli zote kufanyika kwa njia ya Tehama ambayo mifumo hiyo imetengenezwa na wazawa.


 
Mwenyekiti wa Bodi ya Bima ya Afya, Musa Mhimbi alisema wataendeleza mazuri yote yaliyofikiwa ikiwemo kupanua uwigo wa wanufaika na bima ya afya hiyo kutoka asilimia nane ya sasa.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo mstaafu, Anne Makinda alisema mfuko huo ulikuwa na hali mbaya wakaamua kubadilisha mfumo na kufanya marekebisho ya menejimenti na kupunguza idara.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad