Wanafunzi wakimbia shule wakiogopa chanjo ya Corona



Wanafunzi wa shule ya msingi Endiamtu iliyopo Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, walipatwa na hofu ya kupatiwa chanjo ya korona na kukimbia baada ya gari la kubebea wagonjwa la kituo cha afya Mireani kufika shuleni kwao.

Mirerani. Mtafaruku umezuka kwenye shule ya msingi Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara na wanafunzi kukimbia shuleni hapo, mara baada ya gari la kubeba wagonjwa kufika wakihofia kupata chnanjo ya corona.

Wazazi na walezi zaidi ya 30 wenye watoto kwenye shule hiyo walifika mara moja shuleni hapo baada ya kusikia kuwa chanjo ya corona inatolewa kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Hata hivyo, akizungumza na wazazi hao waliofika shuleni hapo leo Ijumaa Julai 30 saa 9 alasiri, Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Evetha Kyara alisema siyo habari za kweli.

Mwalimu Kyara amesema madaktari wa kituo cha afya Mirerani walifika kutoa elimu ya kujikinga na corona na homa ya ini na siyo kutoa chanjo ya corona kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Amesema madaktari hao walifika shuleni hapo kutoa elimu ya corona na kwa walimu wa shule hiyo kwani kila mwaka huwa wanatoa elimu ya afya na walitoa kisha wakaondoka.

“Wanafunzi walipoliona gari na madaktari wamevaa mavazi meupe ndipo baadhi yao wakaingiwa na hofu na kukimbia kwenda majumbani mwao wakidhani wanapata chanjo ya corona,” amesema Mwalimu Kyara.

Amesema wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza na la pili ndiyo waliopatwa na hofu zaidi  na kukimbia huku wakipiga kelele na kusababisha mtafaruku shuleni hapo. 

Mmoja kati ya wazazi wa shule hiyo Baltazari Massawe amesema alipata taarifa kuwa shuleni hapo kuna mtafaruku kutokana na chanjo hiyo, hivyo akafika mara moja shuleni hapo.

“Nina mwanafunzi wa darasa la tano anaitwa Nancy Massawe hivyo nikafika mara moja shuleni lakini kumbe ni habari potofu zilikuwa zinasambazwa na hakukuwa na chanjo ya corona ikitolewa,” amesema Massawe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad