Yanga na Simba Kukiwasha Kesho Uwanja wa Mkapa





AISEE ni kesho buana! Hatimaye imewadia. Ile siku ya watani wa jadi kukutana pale kwa Mkapa. Ni Simba na Yanga kesho Jumamosi.

 

Tambo zimekuwa ni nyingi kwelikweli, na kila upande umeshaanza kutambia kikosi chake. Si unajua kilichotokea pale pambano la awali la Mei 8 lilipoahirishwa?

 

Basi Simba wamekuwa wakitamba kuwa Yanga waliogopa kupeleka timu yao uwanjani kuhofia muziki wa Mnyama, na safari hii wameendelea kuhoji: “Watakuja kweli!

 

”Lakini kwa Yanga, nao wameendelea kujiamini wakisema kuwa wana kikosi imara cha kuifunga Simba na kamwe hawawezi kuiogopa.

 

Awali, pambano hili lilitarajiwa kufanyika Mei 8, mwaka huu lakini liliahirishwa kutokana na sababu ya kusogezwa muda mbele kwa kile kilichotajwa na Bodi ya Ligi pamoja na TFF kuwa ni maelekezo ya serikali.



Lilikuwa lifanyike saa 11, lakini ghafla zikiwa zimebaki takriban saa mbili kabla, ikatoka taarifa kuwa limesogezwa mbele hadi saa 1:00 Usiku, ndipo Yanga wakapeleka timu kwa muda wa awali na Simba wakapeleka kwa muda ulioelekezwa. Ikabidi pambano livunjwe.

 

SASA HATIMAYE LIMEWADIA.

Tayari unaambiwa viongozi na wachezaji wa Yanga leo Ijumaa watakuwa na kikao kizito kwa ajili ya kuujadili mchezo huo.Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ilikuwa nis are ya 1-1 hapohapo kwa Mkapa. Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa Yanga, Dominick Albinus, alisema kuwa kuelekea katika mchezo huo viongozi pamoja na wachezaji wanatarajia kukutana leo Ijumaa kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali.

 

“Ni mchezo ambao tunahitaji kupata matokeo mazuri ambayo ni ushindi, hivyo baada ya kukutana sisi kama viongozi pia tutakutana kwa ajili ya kuongea na wachezaji” alisema kiongozi huyo.

 

Simba chini ya kocha Didier Gomes watakuwa wenyeji wa mchezo huo na wataingia uwanjani kwa kujiamini huku wakiwa na safu kali ya ushambuliaji inayoongozwa na John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu ambao wote kwa ujumla wamefunga jumla ya mabao 35.

 

Katika mabao hayo 35, Bocco ndiye kinara akifanikiwa kufunga mabao 14, akifuatiwa na Kagere na Mugalu waliofunga mabao 11 na 10, mtawalia.

 

Kwa upande wa Yanga chini ya kocha Nasreddine Nabi wao wataingia katika mchezo huo wakiwa wanajivunia ubora wa safu yao ya kiungo inayoongozwa na Mukoko Tonombe, Feisal Salum na Zawadi Mauya.Nabi tangu aanze kuwatumia viungo hao watatu wote kwa pamoja, amefanikiwa kushinda michezo miwili mfululizo ambayo ni dhidi ya Ruvu Shooting 3-2 na dhidi ya Mwadui FC 2-1.

 

Pia Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba, rekodi hiyo ni ile ya Simba kutopata ushindi dhidi ya Yanga katika michezo 3 iliyopita ya ligi huku Yanga wakifanikiwa kushinda katika mchezo mmoja kati ya 3 dhidi ya Simba na miwili wakienda sare.Kuelekea katika mchezo huo Simba watahitaji pointi 3 ili kuweza kutangaza ubingwa jambo ambalo linakoleza moto wa mchezo huo kutokana na Yanga kutokuwa tayari kuona kuwa Simba wanatangazia ubingwa kwao.

 

Afisa Habari wa Simba Haji Manara kuelekea katika mchezo huo, amesema: “Tunawaheshimu wapinzani wetu lakini mechi hii tunahitaji kuchukua pointi 3 ambazo zitatufanya tuweze kuwa mabingwa, kutangaza ubingwa mbele ya Yanga ni raha kwetu na tunatarajia kufanya hivyo ili tuwape furaha kubwa Wanasimba wote.

 

”First eleven ya Simba inayotarajiwa kuanza kesho ni kipa Aishi Manula, Shomari Kapombe, Huseein Mohammed Zimbwe, Joash Onyango, Pascal Wawa, Taddeo Lwanga, Bernard Morrison, Mzamiru Yassin, Bocco, Clatous Chama na Luis Miquissone.

 

Kwa Yanga ni Farouk Shikalo, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Salum Abdallah ‘Fei Toto’, Yacouba Songne, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ na Deus Kaseke.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad