Dar es Salaam. Madaktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji wamesema kirusi cha wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19, kimekuja na mbinu tofauti na za kificho kutokana na dalili zake kuu nne.
Dalili hizo zimetajwa kuwa ni mate kukauka mdomoni, kupata vipele mikononi na miguuni, kuharisha na damu kuganda kwenye mishipa ya moyo kunakosababisha oksijeni kutosambazwa mwilini na hivyo kusababisha kifo cha ghafla.
Akizungumza na Mwananchi jana, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Elisha Osati, alisema kuna mabadiliko yanayoonekana katika dalili mbalimbali za Covid-19 ikilinganishwa na wimbi la kwanza na la pili.
Alisema katika maeneo ambayo wimbi la tatu limetokea kuna wagonjwa bado wanapata dalili za mwanzo, lakini kuna dalili mpya zimejitokeza tofauti na homa, kukohoa, kuchoka, kifua kubana au kupumua kwa shida, ingawa bado kuna wagonjwa wanapata dalili hizo.
“Kumekuwa na dalili za wagonjwa wapya, baadhi ya watu wanapata dalili ya kukauka kwa mdomo, unakuwa mkavu sana pamoja na ulimi kwa sababu hata mate yanakuwa hayatoki vizuri kwa sababu kirusi cha corona kimeonekana kinashambulia baadhi ya tishu na misuli inayozalisha mate iliyopo mdomoni,” alisema.