Agizo la Askofu Ruwai’chi kuhusu chanjo lawaibua mapadri, waumini




“Hiyo ni kauli yake aliyoitoa kama kiongozi wetu, ni nzuri tu na wala haina shida. Ameitoa hadharani na hakuisema kwa ajili ya ubinafsi kwani naye ameshapata chanjo. Moja ya majukumu ya padri ni kulinda watu wake, kuhakikisha wanakuwa salama, hivyo tumeipokea,”.


Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Tadheus Ruwai’chi.
Hivyo ndivyo anavyoanza kusema mmoja wa Mapadri wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alipozungumza na Mtanzania Digital juu ya kauli ya Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Tadheus Ruwai’chi, ya Agosti 22, mwaka huu, ambapo aliagiza mapadri wa jimbo hilo kupata chanjo ya Uviko-19 kwa kuwa ugonjwa huo unaumiza na kuua.

Aidha, wakati Padri huyo ambaye hakuwa tayari jina lake kuanikwa, mwingine aliyetoa maoni yake kwa sharti kama hilo amesema kauli hiyo ya Askofu Ruwai’chi imeeleweka, hivyo kilichobaki ni mapadri kutekeleza tu.

“Sidhani kama nina maoni yoyote kuhusu hilo kwa sababu Baba Askofu akishazungumza siwezi kuhoji alichosema. Nitakuwa naenda kinyume kama nitaanza kusema kwamba…ooh…maoni yangu ni hivi au vile. Nafikiri kwenye kanisa iko wazi,” amesema Padri huyo jijini Dar es Salaam.

Waumini wanasemaje?

Hata hivyo, wakati mapadri wakionesha kukubaliana moja kwa moja na kauli ya Askofu Ruwai’chi, waumini wao wamekuwa na maoni mchanganyiko, ambapo wengine wanasema agizo lake linakiuka maelekezo ya Serikali.

“Kwanza inakiuka maelekezo ya Serikali, kwamba chanjo ni hiari na wala si lazima. Lakini kwa namna nyingine, kauli ya Askofu (Ruwai’chi) inakiuka haki ya mtu kufanya uamuzi juu ya kile anachoona ni sahihi au la.

“Pia, kauli hii inakwenda kugawa waumini. Mfano, kuna mwingine ni muumini na anataka kwenda kanisani lakini hakubaliani na chanjo, hivyo hapo unakuwa unaingilia uhuru wake wa kuabudu,” amesema Esther Haule aliyejitambulishwa kuwa ni mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Janeth Elia mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam, anasema bado watu wamesimama na ile kauli ya mwanzo iliyotolewa na serikali kuwa chanjo hiyo ni hiari.

“Wengi wanajua chanjo ni hiari na si lazima. Mfano kwenye taasisi ninayofanyia kazi, wamesema tuchanje lakini bado kila mtu anasimama na uamuzi wake na hakuna wa kulazimishwa na kazi zinaendelea kama kawaida,” anasema Janeth.

Naye Charles Laurean mkazi wa Sinza, Dar es Salaam, amesema hajajua msimamo wa viongozi wake wa dini kwa maana ya mapadri lakini jambo hilo lilipaswa kubakia hiari ya mtu.

“Sijajua msimamo wa mapadri utakavyokuwa kwa kuwa aliyesema ni kiongozi wao lakini jambo hili lilipaswa kuwa hiari,” amesisitiza.

Askofu Ruwai’ch alisema nini?

Agosti 24, mwaka huu, Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Tadheus Ruwai’chi, ameagiza mapadri wa jimbo hilo kupata chanjo dhidi ya Uviko 19 kwa kuwa ugonjwa huo unaumiza na kuua.

Askofu huyo alitoa agizo hilo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kumuombea aliyekuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Petro na Mkurugenzi wa Tumaini Media, Padri Paul Haule.

Kauli hiyo ya Ruwai’chi imekuja ikiwa ni wiki chache zimepita tangu kuibuka kwa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima aliyedaiwa kuwa chanjo hiyo haifai.


Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima.
Askofu Gwajima ambaye pia ni mbunge wa Kawe jijini Dar es Salaam amekuwa akidai kwamba chanjo za corona zimeundwa kwa kutumia teknolojia ya m-RNA na kwamba zinaweza kubadilisha mfumo wa binadamu jambo ambalo wataalamu wameeleza kuwa siyo sahihi.

Akizungumzia kuhusu kuhimiza watu kuchanja, Ruwai’chi amesema mwaka 2020 wakati wa awamu ya kwanza ya janga la Uviko-19 watu walimuomba Mungu ipatikane chanjo na sasa imepatikana.

“Kama mnavyokumbuka, tulimuomba Mungu ajaalie kupatikana kwa chanjo na sasa imepatikana. Badala ya kutumika, watu wameingia katika malumbano ya kusema haya na yale dhidi ya chanjo.

“Tusingojee hadi mambo haya yatutinge, tutumie vizuri fursa alizotupa Mungu kujikinga na kujihami na kwa sababu hiyo, sijui ni mapdri wangapi ambao mmeshachanjwa.

“Leo naomba nitoe agizo, kila padri akachanjwe, kila padri akachanjwe. Tusifanye utoto, tusifanye lelemama, hii Uviko 19 haina mjomba na shemeji na inatuondolea uhai,” amesema Ruwai’chi na kuongeza:

“Tujihami na tuendelee kumuomba Mungu ili atuhurumie na atuondolee hili janga.”

Utata wa Gwajima

Kwa wiki kadhaa sasa, umekuwapo mvutano mkubwa kati ya Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dorothy Gwajima, chanzo kikiwa ni kiongozi huyo wa dini kuikosoa chanjo kwa madai kuwa ina uwezo wa kubadilisha msimbojeni au chembe za urithi (DNA).

Huku sekeseke hilo likisababisha Mchungaji Gwajima afikishwe Kamati ya Maadili ya Bunge, bado hakuna ushahidi wowote kwamba chanjo za Corona zina athari alizotaja.

Chanjo hizo hazina chembe hai na hazijifungamanishi na jeni za aliyechanjwa na husambaratika wiki chache baada ya mtu kuchanjwa. Pamoja na maneno hayo ya Askofu Gwajima, tayari viongozi mbalimbali wa dini wameshapata chanjo hiyo ya Corona na hadi sasa hakujaripotiwa kuwapo kwa madhara yoyote miongoni mwao.


Takwimu za Chanjo Kwa mujibu wa takwimu za mwisho zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi, Agosti 15, 2021 jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo kwa hiari iliyoanza kutolewa hivi karibuni katika vituo vya kutolea huduma zaidi ya 550 kwa Tanzania bara.

“Tathimini ya zoezi la utoaji chanjo tangu mikoa yote izindue Agosti 4, mwaka huu, inaonesha mpaka kufikia tarehe Agosti 14, 2021, jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo hiyo kwa hiari. Kati ya hao waliopatiwa chanjo, walengwa 121,002 ni wanaume ambao ni asilimia 58 (58.3%) na wanawake ni 86,389 sawa na asilimia 41 (41.7%),” amesema. Mwisho

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad