Watu watano wamepoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea Julai 31 katika eneo la Kasindaga, wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, baada ya basi la abiria kugongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Corora.
Ajali hiyo imeyahusisha gari la abiria lenye namba za usajili T567 DFA mali ya kampuni ya Frester lililokuwa likitoka mkoani Morogoro kuelekea Bukoba mkoani Kagera, ambalo limegongana na gari dogo aina ya Corora lenye namba za usajili T741 AXY lilikuwa likitoka wilaya ya Muleba kuelekea mkoani Geita.
Kwa mujibu wa mganga Mkuu wa hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo Dk. Gresmus Sebuyoya, wamepokea miili ya watu watano, ambayo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo.
Dk. Sebuyoya ametaja majina ya marehemu hao kuwa ni Majid Abubakar, Mdathiru Hashim, Julian Julius, John Method na mwingine amefahamika kwa jina moja la Fravius, wote wanaume.
Naye kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa ajali hiyo na kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo ni uzembe wa dereva wa basi.
"Dereva wa basi alikuwa akiendesha kwa kasi na kusababisha kuhama katika sehemu yake na kwenda kugongana uso kwa uso na gari hilo dogo, na kusababisha vifo vya watu wote watano waliokuwa katika gari hilo," amesema kamanda Malimi.