MHITIMU wa Ualimu ngazi ya Astashahada ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Majengo, Kata ya Ichenjezya wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe amejinyonga na kuacha ujumbe akiwasihi wazazi wake kuzingatia matumizi ya barakoa.
Mwili wa mhitimu huyo ulikutwa unaning’inia juu ya mti, na kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani, mwili huo ulikutwa umeninginia juu ya mti saa moja juzi asubuhi.
Alimtaja marehemu kuwa ni Ezekiel Kitumbo (26), ambayeo alitumia waya wa kusukia umeme kujinyonga na kuning'inia juu ya mti karibu na nyumbani kwao katika Mtaa wa Majengo.
Ngonyani alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa Kitumbo alikuwa na homa kali japo kuwa hukwenda hospitalini kupima na kupata matibabu.
“Baada ya kuupekua mwili wa marehemu mfukoni tuliukuta ujumbe mfukoni uliowasihi wazazi wake kuzingatia matumizi ya barakoa, hivyo mwili baada ya kufanyiwa uchunguzi ulionyesha kuwa alikuwa na homa kali japo haijabainika kama ni ugonjwa gani,” alisema Kaimu Kamanda.
Alisema mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi tayari umekabidhiwa kwa ndugu ili kuendelea na taratibu za mazishi jana katika Makaburi ya Kwa Mzungu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo, Yohana Mapembe alisema tukio hilo wamelipokea kwa masikitiko makubwa kutokana na kijana huyo mhitimu wa chuo cha ualimu mwaka 2019, kutojihusisha na matukio ya hovyo.
“Ezekia Kitumbo ni kijana ambaye alikuwa wa mfano kwa vijana wengi, baada ya kuhitimu Chuo cha Ualimu Singida mwaka 2019 alikuwa anajishughulisha na ufundi pikipiki katika Kata ya Ichenjezya mjini Vwawa,” alisema Mapembe.
Kaka wa marehemu, Regan Kitumbo alisema mdogo wake alionekana kuwa na homa kidogo kwa muda mfupi, lakini hakuwa na tatizo lingine lolote kipindi hicho chote, jambo lililowaumiza baada ya kuukuta mwili juu ya mti juzi.