Alichokisema Rais Samia Mbele ya Kagame




Rais Samia Suluhu Hassan, amesema mazungumzo kati yake na Rais Paul Kagame yamejikita zaidi katika kuimarisha na kukuza uhusiano wa kiuchumi katika nyanja za biashara, uwekezaji na teknolojia ya mawasiliano (Tehama).

 

Rais Samia ameyasema hayo leo jijini Kigali, Rwanda anakoendelea na ziara yake ya kikazi na kuongeza kuwa serikali hizo mbili zimesaini makubaliano na kwamba zitaendelea kuweka uhusiano mkubwa kwenye matumizi ya TEHAMA.

 

“Nawashukuru kwa kuwa nasi bega kwa bega wakati tulichoondokewa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania. Mazungumzo yetu kati yangu na Rais Kagame yalikuwa katika masuala mbalimbali yanayohusu Tanzania na Rwanda.

 

“Namshukuru Rais Kagame kwa kunialika kuja Rwanda, hii ni heshima kubwa kwetu. Napenda kutoa salamu za pole kwako na kwa wananchi wa Rwanda kufuatia janga la tetemeko lililotokea mwezi Mei.

 

“Mazungumzo yalilenga kuimarisha na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati yetu pamoja na mambo mengine ya kisiasa kwenye ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na kwingineko.

 

“Kuna mambo yaliyoingia sasa hivi ya UVIKO-19 ambayo nayo tumezungumza kwa mapana yake, tumeweka mikakati ya kushirikiana kupitia kituo chetu cha Rusumo kwenye mpaka lakini pia kupitia katika mambo kama tulivyosaini ya madawa na mambo mengine.

 

“Kubwa tulilokubaliana ni kukuza ushirikiano zaidi, Tanzania na Rwanda tuko kwenye biashara, uwekezaji na uhusiano mzuri tulionao, hivyo bado kuna fursa nyingi tunazoweza kuzitumia ili kukuza biashara na uwekezaji kwa faida ya pande zote mbili.

 

“Tulizungumzia pia suala la ushirikiano kwenye mambo ya TEHAMA. Tanzania tuna mkongo ambao tumeusambaza katika nchi jirani na Rwanda wanautumia na leo tumesaini hapa makubaliano kwamba tunaendelea kuweka uhusiano mzuri kwenye matumizi ya TEHAMA,” amesema Rais Samia.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad