Askofu Kakobe atangaza msimamo chanjo corona



​​​​​​​ASKOFU wa Kanisa la Full Gospel Bible Felloship (BGBF), Zachary Kakobe, amewataka Watanzania kuacha kusikiliza alichokiita porojo zinazotolewa na baadhi ya watu kuhusu chanjo ya corona, badala yake wawe wanyenyekevu na kuacha kiburi ambacho mwisho wake utakuwa aibu.

Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Felloship (BGBF), Zachary Kakobe.
"Nenda kachanjwe acha kusikia maneno ya porojo porojo hizi, vaa barakoa, tumia vitakasa mikono na maji tiririka, acha kiburi, kiburi cha mtu kitamshusha," alionya Askofu Kakobe jana.

Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni unyenyekevu tu kwa kuwa kipindi hiki binadamu wanatakiwa watumie kilichopo kwa kuwa wakiendekeza kiburi, mwisho wake utakuwa ni aibu.

"Maandiko yanasema kiburi cha mtu kitamshusha. Kwa maana tufanye haya yote ili kusudi la Mungu litimie na sio kinyume chake.

"Yupo mtumishi wa Mungu amepigwa na corona juzi juzi akawa kwenye Oksijeni, tukawa tunamwombea, akawa anasema aliona roho inatenganishwa na mwili, usipende kuona mtu anapata mateso ya corona, ni kusikia tu sababu wewe hujaona, mtu anakwambia mapafu yanawaka moto, ni kama nyuki zaidi ya 1,000 wanashambulia mapafu," alisema.


 
Askofu Kakobe alisema kitendo cha mtu kusema kwamba hawezi kuvaa barakoa eti kwa kuwa ni mtoto wa Mungu au wa mfalme na kuonekana ni zaidi ya wengine, ni kiburi.

"Vijana wengi inakuwa shida, sisi ambao tumekaa muda mrefu kwenye huduma tumenyenyekeshwa kwa mengi, viburi viburi na kujiona mimi ni mimi, huna chochote.

"Maandiko yanasema 'mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za bwana', huna chochote mimi nina imani sana, una imani gani? Maandiko pia yanasema una nini usichokipokea, imani inatokea wapi? Yesu alisema pasipo mimi hamwezi kufanya jambo lolote, hata useme una mamlaka, mamlaka uliyonayo sio yako," alionya.


Aliongeza kuwa kama ungekuwa na mamlaka yako, basi yeyote unayetaka kumfufua ungemfufua na yeyote unayetaka kumponya, ungemponya lakini sivyo.

"Mwanangu nenda kachanjwe haraka, mtumishi wa Mungu nenda kachanjwe, bado Mungu ana kazi na wewe, hujaimaliza, anataka akutumie wewe ili uweze kuwasaidia watu wengine," alisema.

Askofu Kakobe alisema hivi sasa watu wameanza kusema wameanza kuweka 'busta' kwamba sasa hata mtu aliyepigwa chanjo ya kwanza na ya pili imekuja nyingine.

Alisema hata kama zingekuwa chanjo ngapi, wewe chanjwa tu kwa kuwa hazipunguzi chochote.


 
"Tunameza vidonge mara ngapi na kubadilisha dawa mara ngapi kwa ajili ya tatizo ambalo halijaondoka?" alihoji

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad