Bunge limepunguza muda wa kuanza kwa vikao vyake ambapo sasa litaanza vikao vyake kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 1:00 usiku huku kukiwa hakuna kipindi cha maswali na majibu asubuhi ikiwa ni jitihada za kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Agosti 31, 2021 na Spika wa Bunge, Job Ndugai mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika bungeni.
“Lengo ni kupunguza muda wa kukaa pamoja. Kuanzia kesho kikao kitaanza saa 8:00 mchana na kumalizika saa 1:00 jioni, hii itatufanya tutumie saa tano badala ya saba na nusu ambao ni utaratibu wa kawaida,”amesema.
Amesema pia kipindi cha maswali na majibu kitakuwa cha dakika 60 badala ya dakika 90 unaotumika kwa kawaida bungeni.
Wabunge wakiwasili katika viwanja vya Bunge Dodoma kwa ajili ya kuanza kwa kikao cha Bunge.Picha na Said Khamis
Ndugai amesema kwa lengo la kupunguza msongamano bungeni watatumia kumbi mbili wakati wa vikao bungeni ikiwa ni ukumbi wa Bunge na ule wa Pius Msekwa.
“Ukumbi wa Msekwa utawawezesha kuwafanya wabunge watakaoshiriki katika kikao cha Bunge kushiriki sawa na wale waliopo katika ukumbi wa Bunge,”amesema Ndugai.
Amesisitiza wabunge kuvaa barakoa katika kipindi chote wanachokuwa katika viwanja vya Bunge hususan katika kumbi za Bunge.
Hata hivyo, amesema wale wenye tatizo la kiafya linalowafanya wasivae barakoa wataruhusiwa baada ya kupata idhini yake.
Kuhusu wageni, Ndugai amesema hawataruhusu wageni wanaofika kutembelea Bunge wala mafunzo na kwamba watakaoruhusiwa ni wale wenye shida za kiofisi, maofisa wa Serikali wanaofuatilia shughuli za Bunge na waandishi wa habari.