Dodoma. Ofisi ya Bunge imekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa wabunge ambao hawatachanja chanjo ya corona hawataruhusiwa kuingia bungeni.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Agosti 14, 2021 na ofisi ya imeeleza kuwa taarifa hizo niupotoshaji na hazina ukweli wowote.
“Tunapenda kuujulisha umma kwamba, taarifa hizo hazina ukweli wowote kwani maelekezo yaliyopo na ambayo Spika wa Bunge, Job Ndugai amekuwa akisisitiza na kuwahimiza wabunge kujitokeza kuchanja chanjo hiyo kwa hiari yao,” imesema taarifa hiyo.
Hata hivyo taarifa hiyo imesema, Ofisi ya Bunge imeandaa utaratibu utakaowawezesha Wabunge wote kupata chanjo hiyo katika viwanja vya Bunge kwa hiari yao wenyewe.
Wabunge wamesisitizwa kutumia hiyari hiyo kujitokeza ili kupata chanjo kwa ajili ya kujikinga na kuwakinga wengine katika gonjwa hilo.
Bunge ni sehemu mojawapo yenye mikusanyiko ya watu wengi wakiwemo wabunge, watumishi wa bunge, askari, waandishi wa habari na wageni ambao hutembelea kwa ajili ya kujifunza.