Chama cha Mapinduzi kimesikitishwa na upotoshwaji mkubwa uliyofanywa na gazeti la Uhuru toleo Namba 24084 la leo Jumatano tarehe 11 Agosti, 2021. Gazeti hilo limepotosha sehemu ya mahojiano aliyofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC ,Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika habari yake kuu limeandika kichwa cha habari “Sina wazo kuwania urais 2025- Samia” Huu ni upotoshwaji mkubwa na kumlisha maneno Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan hakusema kabisa maneno hayo. Hili ni kosa kubwa linalokwenda kinyume na sera inayoongoza vyombo hivyo, jambo ambalo halitavumiliwa hata kidogo hivyo HATUA KALI za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika katika uandaaji wake.
Gazeti la Uhuru ndiyo “Adam na Hawa” wa magazeti yote hapa nchini, linawajibika kuonesha weledi wa hali ya juu na sio vinginevyo.
Tunawaomba wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na watanzania kwa ujumla kupuuza habari hiyo kwani imeandikwa na watu wenye maslahi yao binafsi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan fikra na nguvu zake kwa sasa zimejikita katika kuwatumikia watanzania na si vinginevyo.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi.
Shaka Hamdu Shaka
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
Itikadi na Uenezi
11 AGOSTI, 2021.