Daktari Aliyeishiwa Nguvu Kwenye Mdahalo Afunguka Kilichotokea




Daktari Aliyeishiwa Nguvu Kwenye Mdahalo Afunguka Kilichotokea

DAKTARI aliyeishiwa nguvu wakati akitoa mada kwenye mdahalo Dk Sospeter Bulugu amefunguka na kusema alipatwa na tatizo la kushuka kwa sukari kwenye damu ambayo kitaalamu inajulikana kama Hypoglycemia.

 

Bulugu amesema kuwa wakati akizungumza alipata hali ya kizunguzungu ambayo hata yeye hakuielewa baada ya wataalamu kumuangalia akiwemo Dk Kaushik na timu yake walimpa huduma ya kwanza na baada vipimo ilionekana sukari yake imeshuka.

 

Mtaalamu huyo ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa Agosti 13, ambapo amesema alipatiwa vinywaji vyenye sukari na chakula na baada ya hapo hali yake ikawa vizuri na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

 

Mtoa mada huyo ambaye ni Kamishna wa Afya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (Tahliso) alikuwa akitoa mada kuhusu uelewa wa vijana juu chanjo ya Covid-19 katika mdahalo wa kitaifa kisayansi uliofanyika jana.

 

Ufafanuzi huo umefuatia baada ya video fupi kusambaa mitandaoni ikimwonyesha daktari huyo akipatwa na hali ya kizunguzungu hivyo, wataalamu kulazimika kumpatia huduma ya kwanza na baadaye ilisikika sauti ya waziri ikihoji baadhi ya maswali iwapo alikuwa amepata chanjo.

 

Kwenye video hiyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima amesikika akihoji iwapo Dk Bulugu alikuwa amepata chanjo na ilipothibitika hakupata ya Uviko-19 sauti ya Waziri wa Afya ilisikika tena ikisema, basi amepatwa na kushuka kwa sukari hasa ukizingatia tangu kuanza kwa mkutano huu hakukuwa na mapumziko ya chai.

Wakati huohuo Wizara ya Afya imetoa ufafanuzi kuhusu suala hilo na kusema uchunguzi umeonyesha aliishiwa sukari kwenye damu.

 

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Agosti 13, 2021 na Mganga Mkuu wa Serikali Dk Aifelo Sichwale imeeleza kuwa uchunguzi ulionyesha kuwa hali hiyo ilitokana na kushuka kwa sukari kwenye damu ambayo kitaalamu inajulikana kama Hypoglycemia.



Dk Sichwale amesema katika mdahalo huo jumla kulikuwa na wawasilisha mada 20 ambapo, Dk Bulugu alikuwa mmojawapo wa wawasilisha mada akiwa mzungumzaji wa mwisho.

 

Amesema baadae Waziri alielekeza apewe huduma ya kwanza ikiwemo kinywaji chenye sukari na pipi ambapo, baada ya hapo hali yake ilitengemaa.

 

“Wakati tukio hilo likitokea ilibainika kuwa vyombo vya habari vilikuwa vikichukua tukio hilo jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kitabibu pale mteja anapokuwa anapatiwa huduma kwenye mikono ya kitaalam huku akiwa hajaridhia huduma hiyo iwe wazi.

 

“Hivyo kwa kutumia kiapo na maadili ya taaluma yake kama daktari Waziri aliwataka wanahabari wasichukue tukio hilo lakini, imebainika kuwa wapo waliochukua na kuzisambaza na matokeo yake zimetumika kupotosha vikihusisha tukio hilo na madhara ya chanjo, jambo ambalo siyo kweli,” amesema.


Dk Aifelo amesema katika eneo la ukumbi huo hakukuwa na zoezi la uchanjaji na Dk Bulugu hajawahi kuchanjwa chanjo ya Covid -19.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad