Dar/Morogoro. Baada ya Mwananchi kuripoti habari kuhusu mjamzito aliyejifungua ndani ya bajaji baada ya kukosa huduma katika kituo cha afya Mikumi mkoani Morogoro, Waziri wa Afya, Dk Doroth Gwajima ameingilia kati.
Taarifa iliyotolewa juzi na Kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini – Afya, Catherine Sungura, ilieleza kuwa Waziri Gwajima ameuelekeza uongozi wa mkoa, ufanyie kazi sakata hilo na kwamba anahitaji taarifa hiyo aipate ndani ya siku saba.
Mjamzito huyo Jenifa Antony alipatwa na mkasa huo Aprili mwaka huu, baada ya kukosa huduma kutokana na kushindwa kulipa Sh120, 000 zilizotakiwa na daktari kinyume na utaratibu.
Wakati tukio hilo likitokea, utafiti wa Shirika la afya duniani (WHO) uliochapishwa mwaka 2019 unaonyesha theluthi moja ya wanawake katika nchi za kipato cha chini, wameripoti kukumbwa na mateso kipindi cha ujauzito.
Tukio hilo ambalo kwa mara ya kwanza liliibuliwa Julai 27 mwaka huu na Abadallah Kasanda katika mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela, kuhamasisha wananchi kupokea Mwenge wa Uhuru katika mji mdogo wa Mikumi.
Kasanda aliwasilisha kero hiyo akisema ilimtokea mkewe na akajifungulia kwenye bajaji kwa kukosa huduma, baada ya kukataa kutoa Sh120,000 kinyume na utaratibu.
Shigela baada ya kupokea malalamiko hayo aliamuru kukamatwa kwa Dk Cassius Rwebangira anayetuhumiwa kwa kosa hilo.
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa, Jenifa alifikishwa hospitalini hapo Aprili 22, mwaka huu, saa 5 usiku baada ya kupata uchungu, kabla ya mambo hayajakwenda kinyume na matarajio yake.
Akisimulia mkasa huo, Kasanda alisema: “Baada ya mke wangu kupata uchungu, saa 5 usiku tulimpeleka kituo cha afya Mikumi na akalazwa usiku ule. asubuhi ya Aprili 23 nesi wa zamu alinifuata na kuniambia njia imefunguka, hivyo atajifungua mtoto kwa njia ya kawaida,” alisema.
Lakini ilipofika saa 4 asubuhi, Kasanda alisema daktari wa zamu, Dk Rwebangira alimuita na kumpa taarifa tofauti, akimweleza kuwa mkewe angejifungua kwa njia ya upasuaji.
Alisema daktari huyo alimtaka ampatie Sh120,000 ili atumie vifaa vyake kwa ajili ya upasuaji huo, badala ya kwenda kuvinunua sehemu nyingine.
Alisema alipohoji, daktari alimtaka aachane na maneno ya nesi na amsikilize yeye kwa kuwa ndiye daktari.”
Baada ya kupewa majibu hayo, Kasanda alitoka kujadiliana na ndugu yake kuhusu kauli ya daktari na namna gani watapata fedha hizo.
Baada ya majadiliano hayo, alirejea kwa Dk Rwebangira na kumweleza hawana uwezo wa kupata fedha hizo wakati huo na kuwa kama ingeshindikana, aruhusu uhamisho na ndipo mjamzito huyo alipojifungua akiwa njiani