Pep Guardiola amesema kuwa ataondoka Manchester City mkataba wake utakapomalizika mnamo 2023 - na anatarajia kuifundisha timu ya taifa.
Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 50, aliyejiunga na City mwaka 2016, amepanga "kupata mapumziko" baada ya miaka saba akiifunza klabu hiyo ya Ligii Kuu Uingereza.
"Nadhani nitasimama. Nitalazimika kupumzika, angalia kile tumefanya," Guardiola alisema.
"Hatua inayofuata itakuwa timu ya taifa, ikiwa kuna uwezekano."
Akizungumza kwenye hafla iliyofanyika kwa njia ya mtandao iliyoandaliwa na kampuni ya huduma za kifedha ya Brazil XP Investimentos, na kunukuliwa na ESPN Brasil, aliongeza: "Ningependa kufundisha timu ya Amerika Kusini, Ulaya, inayocheza Copa America, nataka kuwa na uzoefu huo.
" Habari hiyo ilikuja kama pigo kwa City siku hiyo hiyo ambayo mbio zao za kumsajili mshambuliaji wa Tottenham Harry Kane zilifikia kikomo huku nahodha huyo wa England akithibitisha kuwa atasalia na klabu yake.
Guardiola, ambaye ameshinda mataji matatu ya Ligi ya Primia, Kombe moja la FA na makombe manne ya Ligi akiwa na City, alichukua mapumziko ya miezi 12 baada ya kuondoka Barcelona mnamo mwaka 2012 kabla ya kujiunga na Bayern Munich.